Habari za Punde

TAMWA - ZNZ yaunga mkono uundwaji wa Wizara ya wanawake pekee

 
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania - Zanzibar (TAMWA, ZNZ), kinashukuru kwa dhati maamuzi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi ya kuunda Wizara maalum itakayoshughulikia pamoja na mambo mengine, masuala  ya Wanawake na kwa muktadha huo, kuwa ni Wizara inayojitegemea, nje ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kama ilivyokuwa awali. 

Hali hiyo itapelekea masuala ya wanawake kuweza kushughulikiwa kwa makini zaidi ikiwa ni pamoja na kutengewa raslimali inazostahiki ili kuhakikisha mipango, utekelezaji na ufuatiliaji unafanyika kama inavyostahiki.
Pendekezo la kuwa na Wizara za wanawake pekee, lilikuja katika mikutano ya kimataifa ya wanawake hasa uliofanyika Nairobi mwaka 1985 kufuatia dhuluma ambazo wanawake wamekumbana nazo na zilivyowafanya kuwa nyuma katika nyanja za kimaisha, hivyo Wizara ya wanawake pekee ilishauriwa ili inyanyue hali hizo za wanawake duniani kwa ujumla na nchi zinazoendelea kwa upekee hasa kama Zanzibar ambayo imezongwa zaidi na mifumo kandamizi dhidi ya wanawake na watoto wa kike.  
TAMWA - ZNZ pia kinampongeza Waziri Riziki Pembe aliyeteuliwa kuiongoza Wizara hiyo kutokana na uwezo wake na uzoefu, TAMWA tunaamini ataweza kuleta mabadiliko yanayostahiki.
Hivyo, TAMWA ZNZ inapenda kumshauri Mh. Waziri kuweka mifumo madhubuti ya kurikodi maendeleo ya wanawake katika nyanja za kiuchumi na kiuongozi kwa vile bado hazijaratibiwa vizuri. 
Hivi sasa kuna jitihada nyingi za kuinua kipato cha wanawake lakini bado hakuna mifumo mizuri kuonesha hasa mabadiliko yanayotokea na mapungufu yaliyopo ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa. Kukiwa na takwimu maalum za wanawake hao itakuwa ni rahisi kuonesha maendeleo yaliyofikiwa katika kundi hilo muhimu ambalo linafanya zaidi ya asilimia 50 ya wakaazi wote wa Zanzibar.
Pia katika uongozi, takwimu za wanawake katika nafasi mbali mbali za kiutendaji katika ngazi za kitaifa na shina zikiwemo kwenye Wakurugenzi, miundo ya bodi/kamati za kiutendaji bado ni changamoto kuzipata pamoja na kuwa nchi inatekeleza itifaki na maazimio mbali mbali ya kuleta usawa wa kijinsia hasa katika uongozi.
Itifaki ya Umoja wa Afrika (AU) ya mwaka 2003 na Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC) ya mwaka 2008 zote zinahimiza asilimia 50/50 katika vyombo vya maamuzi katika Nyanja zote hizo bila ya takwimu na mikakati maalum haitakuwa rahisi kupima muelekeo wa nchi katika hilo.
Mwisho tunamtakia kila la kheir Waziri wa Wanawake katika kutekeleza majukumu yake na kuwaomba wadau wa wanawake na jamii kwa ujumla kumpa mashirikiano ili kufikia malengo yaliyowekwa. 

Dkt Mzuri Issa,
Mkurugenzi,
TAMWA, ZNZ

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.