Habari za Punde

Waziri Mhe.Hamza Hassan Akabidhi Magari Matano kwa TASAF Zanzibar.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais  Sera, Uratibu  na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma  akimkabidhi funguo na gari tano, Mratibu wa TASAF Unguja, Makame Ali Haji,  Magari kutoka Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya Matumizi ya  Shughuli za TASAF makabidhiano yaliyofanyika  katika Ofisi za TASAF, Mazizini. (PICHA NA OMPR)

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imehimiza umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya wananchi wake ili kufikia malengo iliyojiwekea.

Aidha, imewataka watumishi kutoka sekta za umma na binafsi kudai risiti za mashine wakati wote wanapofanya matumizi ya mahitaji yao kwa lengo la kunusuru fedha za serikali zisipotee.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya gari tano kwa uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii, TASAF huko ofisi za mfuko huo, Mazizini mjini Unguja, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera na Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma alisema fedha zilizotumika kunununulia gari hizo ni za serikali ya Jamuhuri ua muuungano wa Tanzania ambayo imekopa kutoka benki ya dunia.

Alisema serikali ndie inalipa fedha hizo, kupitia kodi wanazolipa wananchi, hivyo aliwataka wananchi kudai risiti za mashine kila wanaponunua mahitaji yao.

“Tunaponunua bidhaa, lazima tupatiwe risiti, tunapofanikiwa kudai risiti fedha zinazopatikana kupitia risiti hizo zinakwenda kulipa deni la magari haya, sababu hili ni deni la serikali, ni deni la wananchi”

“Kila mtu akienda dukani kununa chochote lazima adai risiti ya mashine, na hili ni agizo la serikali hata kwa watumishi wa umma kila wanapofanya malipo lazima wadai risiti ili fedha hizo zikalipe deni la magari haya” alilisisitiza Waziri Hamza

Aidha, alieleza fedha za serikali ni fedha za wananchi na kuongeza kuwa wananchi wanashiriki kulipa mkopo huo kupitia kodi wanazozilipa wanapodai risiti.

Aliwataka watumishi waserikali kuwa mfano mzuri kwa wananchi kwa kudai risiti za mashine ili nao wawe wepesi kwa kudai risiti.

Akizungumzia suala la ongezeko la mishahara kupitia ahadi ya Rais wa Zanzibar kwa watumishi wa umma, Waziri Hamza alisema kudai risiti kwa bidhaa zinazouzwa ni kulipia kodi kwa kudai risiti kutaisaidia serikali kukusanya mapato yanayokwenda kulipa mishahara ya watumishi wake, kununuliwa nadawa na mahitaji mengine ya maendeleo ya nchi.

Hata hivyo alisema serikali imesamehe baadhi ya kodi kwa lengo la kuwapa ahuweni wananchi wake na kutolea mfano kodi za mafuta.

Kwa upande wa magari hayo Waziri Hamza aliueleza uongozi wa TASAF kwa kuwapa agizo kutoka kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba magari hayo yakatumiwe kwa lengo lililokusudiwa na si vyenginevyo.

“Magari haya yaendelee kuwahudumia wananchi na sio matumizi ya utashi wa mtu binafsi”

Nae Katibu Mkuu Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Thabit Idarous Faina alisema mbali ya kukabidhiwa gari tano kwa matumizi ya Unguja na Pemba na kuongeza kuwa Mradi wa TASAF  pia umekabidhiwa vifaa vyengine vya kazi zikiwemo mashine za fotokopi ambavyo kwa mapaja na magari hayo vinagharimu jumla ya milioni 394.

Akizungumzia changamoto katika kuwafikiwa walengwa wa mradi wa TASAF, Katibu Faina alieleza kwa kaiwaida walengwa hao wanatakiwa kufikiwa kila mwezi lakini kutokana na changamoto ya awali ya usafiri walifikiwa kila baada ya miezi miwili.

Jumla ya wanufaika 32,523 kwa Zanzibar wamefikiwa na mradi wa TASAF ambapo matarajio ya kuzifikia elfu 50 kutoka shehia 388 za Unguja na Pemba kwa lengo la kuwakwamua na ukali wa umasikini.

Imetayarishwa na kitengo cha habari na mawasilinao, OMPR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.