Habari za Punde

Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria Zanzibar.

Wasaidizi wa Sheria wakionesha vipaji vyao kwa Igizo lenye maudhui ya uwajibikaji wa Wasaidizi wa Sheria katika Hafla ya Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria Zanzibar iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF Lulu Ng ‘wanakilala akitoa salamu za Shirika la LSF katika Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria Zanzibar yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Harun Ali Suleiman akizungumza katika maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Harun Ali Suleiman akizungumza katika maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiagana na Viongozi mbali mbali baada ya kukamilika kwa Maadhimisho ya wiki ya Msaada wa Kisheria Zanzibar yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni.

Na.Abdulrahim Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka wasaidizi wa Sheria Nchini kuendelea kuhamasisha Jamii katika masuala mbali mbali ya Kisheria ili kupunguza matendo maovu Nchini.

Mhe. Hemed ametoa Wito huo katika maadhimisho ya Tatu ya Wiki ya Msaada wa kisheria Zanzibar yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar. 

 

Amesema juhudi zinazochukuliwa na wasaidizi hao ni za kupongezwa na kuwataka wasaidizi hao kuongeza kasi mijini na vijijini kwa kuhamasisha uwepo Sheria hasa utoaji wa ushahidi kwenye kesi za udhalilishaji. 

 

Ameeleza kuwa bado jamii inakumbwa na changamoto ya uelewa Mdogo wa utoaji wa ushahidi hasa vijijini katika kesi za udhalilishaji hivyo kufika kwao kwenye maeneo hayo kutasaidia kumaliza changamoto hiyo.

 

Mhe. Hemed ameziagiza Mamlaka zinazosimamia ushahidi kuhakikisha wananchi hawapati usumbufu wa aina yoyote wanapoitwa kwa kutoa ushahidi hasa kuzingatia baadhi hukaa  muda mrefu bila ya mafanikio.

 

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali haifurahishwi kuona kesi zinachelewa kukamilika kwa kisingizio cha kutokamilika kwa upelelezi na kuzitaka Mamlaka husika kusimamia upelelezi wa kesi ili zikamilike kwa wakati na kuzingatia haki.

 

"kuendelea kuwa na mrundikano wa kesi ambazo zinaelezwa kuwa upelelezi haujakamilika hili halina tija na halileti sura nzuri kwa Nchi"

 

Aidha Mhe. Hemed amewasisitiza Wanasheria kusimamia haki nchini ili wananchi wawe na Imani na Serikali yao jambo ambalo ni miongoni mwa  ahadi za Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kipindi akiomba ridhaa za wazanzibari. 

 

Hata hivyo ameeleza kuwa kutokuwepo suala la  utoaji haki kunasababisha kuchelewa kwa maendeleo Nchini.

 

Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Harun Ali Suleiman ameutaka Uongozi wa Skuli ya Sheria Zanzibar kuandaa mafunzo kwa wasaidizi wa Sheria kwa kushirikiana na Shirika la Msaada wa Kisheria (LSF) ili kuongeza ujuzi kwa wasaidizi hao na wazidi kufanyakazi uzuri na kujiamini.

 

Aidha Mhe. Harun amesema Kesi za Udhalilishaji zinakithiri kila siku ambapo jamii inahitaji nguvu za ziada ili kuongeza uelewa kwa Jamii na kusimamia haki.

 

Kwa Upande wake Mkurugenzi Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Hanifa Ramadhan Said ameeleza kuwa wiki ya Msaada wa Kisheria ni muda muwafaka kwa wasaidizi wa kisheria kukaa pamoja na Taasisi mbali mbali kujitathimini kujua   namna walivyofanikiwa katika kuisaidia jamii.

 

Aidha Bi Hanifa amesema tokea kuasisiwa kwa Idara hiyo wamekuwa karibu zaidi na wasaidizi wa Sheria na kuwataka wasaidizi hao kuendelea kuwajibika ili kufikia lengo lililokusudiwa.

 

Nae Muwakilishi wa Watoaji Msaada wa kisheria Ndg. Shaban Sarboko ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kwa kuendelea kuwaunga Mkono katika harakati zao za kuitumikia Jamii.

 

Aidha ameeleza kuwa licha ya uwajibikaji wao bado wanakabiliwa na Changamoto mbali mbali ikiwemo ukosefu wa Rasilimali watu, vifaa pamoja na Ofisi ambazo zinapelekea kuwa kikwazo katika kazi zao za kila siku.


Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

09/07/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.