Habari za Punde

Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi yapamba moto

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. George Simbachawene akizungumza katika Mkutano wa sekta binafsi uliohusu uchangiaji wa rasilimali kwa ajili ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 uliofanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam Agosti 15, 2022.

Na. Mwandishi wetu

Serikali imesema maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi yamefika zaidi ya asilimia 95 hivyo ni vyema kuendelea kushirikiana kwa pamoja kwa kuzingatia muda uliobaki ili kulifikia lengo lililopo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene katika Mkutano Maalum wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alipokutana na sekta binafsi kwa lengo la kutambua mchango wao katika kuelekea siku hiyo ikiwemo ya rasilimali fedha, huduma na vifaa kwa ajili ya zoezi la Sensa ya watu na makazi ya Mwaka 2022.

Alisema kuwa, Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi hivyo ni vyema kwa kila mdau kushirikia katika zoezi hili  kwa kadri awezavyo kwa kuchangia  rasilimali fedha, huduma na vifaa vitakavyosaidia kufanikisha zoezi la sensa.

“Karibu kila mdau ameshiriki katika maandalizi ya sensa kupitia taasisi ya sekta binafsi (TPSF) na tumekutana hapa ili kuonesha mshikamano wetu na kutambua michango yenu ninawapongeza sana," alisema Simbachawene.

Naye katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu amesema serikali imeshirikiana sekta binafsi  katika maandalizi ya kuelekea siku ya sensa kwa namna mbalimbali ikiwemo, kugharamia matangazo yanayotoka kwenye vyombo vya habari.

“Kampuni za simu zilisaidia kutoa ujumbe mfupi wa kuhamasisha wananchi na kuelimisha wananchi juu ya zoezi la sensa ya watu na makazi na baadhi kuahidi kuchangia fedha na vifaa mbalimbali ili kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi” alisisitiza Dkt. Jingu

Naye Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Mhe. Anne Makinda ameshukuru sekta binfasi kwa mchango wao katika kuwezesha maandalizi ya kuelekea siku ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 Agosti, 2022.

“Tumejipanga kusimamia matumizi yote tunayopewa na kuhakikisha tunapata matunda tunayotegemea.” aliesema Mhe. Makinda

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.