Habari za Punde

Wafugaji Waikubali Teknolojia ya Uhimilishaji.

Na Mbaraka Kambona, Arusha

Wafugaji wanaofanya shughuli zao Mkoani Arusha wamesema teknolojia ya uhimilishaji wa mifugo hususan Ng'ombe inayotolewa na Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC USA RIVER) ni bora na  imeleta mapinduzi makubwa katika uboreshaji wa koosafu za Mifugo yao.

Wakiongea kwa nyakati tofauti katika Maonesho ya Wakulima NaneNane kwa Kanda ya Kaskazini yanayofanyika Mkoani humo Agosti 3, 2022, Wafugaji hao walisema  mbegu za madume bora  ya Ng'ombe zinazozalishwa katika kituo hicho ni nzuri kwani tangu waanze kuzitumie kupandikiza kwa Ng'ombe wao imesaidia kuboresha koosafu huku uzalishaji wa maziwa na nyama ukiongezeka maradufu tofauti na hapo awali.

Mfugaji kutoka Tengeru, Mkoani Arusha, Bw. Ayoub Urio alisema kuwa kituo cha NAIC kina mbegu bora za madume ya Ng'ombe na hivyo aliwahimiza  wafugaji wengine ambao bado wanahimilisha mifugo yao kwa njia ya asili waache kufanya hivyo na watumie mbegu za NAIC.

Aliongeza kwa kusema kuwa Mwaka 2021 alipata kiasi cha Shilingi Milioni Sita na Elfu Thelathini baada ya kumuuza dume moja wa Ng'ombe ambaye mbegu yake aliipata kutoka NAIC.

Alifafanua kuwa huduma ya NAIC imesaidia sana kupunguza gharama za kupata madume bora  kwani aina za mbegu wanazozalisha ukisema uagize  kutoka nje ya nchi gharama yake ni kubwa kiasi kwamba mfugaji mdogo hawezi kuimudu.

Naye Mfugaji kutoka Kijiji cha Lole, Mkoani Arusha, Bw. Ebenezer Mrema alisema kuwa tangu aanze kutumia mbegu za NAIC Ng'ombe wake wanatoa Lita 30 kwa siku hivyo wafugaji wazitumie mbegu hizo na Mafanikio watayaona.

Kwa upande wake, Mtafiti Mkuu kutoka Kituo hicho cha NAIC alisema kuwa kwa mwaka 2021/2022 wamefanikiwa kuhimilisha  ng'ombe wasiopungua Sabini Elfu ( 70,000).

Aliongeza  kwa kusema kuwa wanawakaribisha vijana waliomaliza masomo kuanzia kidato cha Nne  na kuendeleza waende kujifunza kuhusu teknolojia hiyo ya upandikiza wa mbegu bora za madume ya Ng'ombe kwa njia ya mirija ili wafugaji wengi nchini wawe na mifugo bora na yenye tija kwao na Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.