Habari za Punde

Serikali Imeanza Mchakato wa Kuimarisha Maslahi ya Watendaji katika Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Charles E. Kichere (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo,5-9-2022 (kulia kwake) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt.Othman Abass Ali, wakiwa na ujumbe wao
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Charles E. Kichere (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo,5-9-2022 (kulia kwake) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt.Othman Abass Ali
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Charles E. Kichere (kulia kwa Rais) baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 5-9-2022, na (kushoto kwa Rais) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt.Othman Abass Ali

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imeanza mchakato wa kuimarisha maslahi ya watendaji katika Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Serikali, ili  kulinda nguvu kazi iliopo.

Dk. Mwinyi amesema hayo ikulu Zanzibar, alipozungumza na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Charles E. Kichere, ambapo pamoja na mambo mengine amefika kwa ajili ya kujitambulisha.

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa kazi inayofanywa na watumishi hao (Wakaguzi) na kusema tayari  mchakato wa kuimarisha maslahi yao umeanza  kuambatana na mfumo uliopo wa makundi, akitolea mfano wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA) inayopaswa kuwa katika kundi la taasisi zinazozalisha kama vile Bandari.

Alisema kuna umuhimu wa kuondoa tatizo la kimaslahi kwa watendaji wa taasisi hiyo kwa kuzingatia kuwa wengi wa watu wanaokaguliwa  wana maslahi makubwa, hivyo kuwepo uwezekano wa kuondoka na kwenda kutafuta maslahi makubwa maeneo mengine.

Akigusia ukaguzi wa Vyombo vya Muungano viliopo Zanzibar, Dk. Mwinyi alisema anafarijika kuwepo kwa mashirkiano ya taasisi mbili za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Tanznaia na ile ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar , huku akibainisha kuwepo changamoto kubwa katika vyombo hivyo kuwa  havikaguliwi au havikaguliwi vizuri.

Alisema kuna matatizo makubwa katika Idara ya uhamiaji Zanzibar, “kuna wakati ilitumwa Kamati kwenda kufanya ukaguzi na kugundua kiasi cha shilingi Bilioni nane zilikuwa zimepotea ndani ya miezi sita, bado kuna kazi ya kufanya”.

Alisema kuna uwezekano wa vyombo hivyo vya Muungano vinavyofanya kazi hapa zanzibar kujificha nyuma na kutokuwemo katika ukaguzi, jambo alilosema linapaswa kurekebishwa, akibainisha hatua ya taasisi hizo kufanya kazi kwa pamoja kutasaidia juhudi hizo.

Aidha, alipongeza ukaguzi wa hivi karibuni kuwa  umeondokana na ukaguzi wa vitabu na badala yake kwenda kwenye miradi ili kuona uhalisia.

‘Kuna watendaji hodari wa kuandika vitabu katika baadhi ya taasisi’ alisema.

Alisema Zanzibar inaelekea kwenye sekta ya Mafuta na Gesi Asilia, hivyo kuna mambo mengi ya kujifunza kutoka Tanzania Bara ambayo tayari imepiga hatua katika sekta hiyo, sambamba na kuwepo umuhimu wa kuwajengea uwezo watendaji (wakaguzi).

Aidha, alisema anafarijika na mashirikiano makubwa yaliopo kati ya taasisi hizo, jambo ambalo amekuwa akilitilia mkazo kwa kuzitaka taasisi za Zanzibar kuchota uzoefu kutoka Taasisi zinazofanana Tanzania Bara.

Nae, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (CAG) Charles E. Kichere alimpongeza Dk. Mwinyi kwa kazi kubwa na maono yake katika kuiletea Zanzibar maendeleo pamoja na kusimamia rasilimali za nchi.

Alisema jukumu la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni kumsaidia Rais kwa kufuata Dira kupitia nyanja mbali mbali za kiuchumi na kimaendeleo.

Alieleza kuwa taasisi CAG Tanzania pamoja na ile ya CAG Zanzibar  zimekuwa na mashirikianao mazuri, ambapo baadhi ya nyakati huunganisha nguvu katika utekelezaji wa majukumu hususan katika miradi mikubwa pamoja kujengeana uwezo.

Alisema taasisi hizo kama zilivyo sawa katika utekelezaji wa majukumu yake, zinakabiliwa na changamoto zinazolingana, ikiwemo ile ya maslahi, hivyo akaziomba Serikali zote mbili kuangalia uwezekano wa kuondokana na changamoto hiyo.

Mapema, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar Dk. Othman Abassa alisema kumekuwepo ushirikiano mkubwa kati ya taasisi hizo mbili, akitolea mfano wa hatua za hivi karibuni, ambapo Ofisi ya CAG Tanzania ilIisaidia CAG Zanzibar kufanikisha Ukaguzi katika taasisi za Muungano, ikiwemo  BOT , TRA na Ofisi za Mabalozi , pale ilipokuwa ikiendesha zoezi la ukaguzi kwa kuwawezesha watendaji wake kufika hadi Mikoa ya Tanzania Bara, sambamba na kusomesha watendaji kutoka Ofisi ya CAG Zanzibar, gharama zikitolewa na  Ofisi ya CAG Tanzania.

Alisema katika kipindi kifupi kijacho, taasisi hizo zinatarajiwa kukamilisha mchakato wa utiaji saini hati za mashirikiano (MoU).

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano Ikulu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.