Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Akagua Ujenzi wa Barabara ya Mzunguko wa Nje wa Jiji la Dodoma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza  Kaimu Meneja wa Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS ) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi  Salome Kabunda ( kushoto) ambaye alikuwa akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi  kwa kiwango cha lami wa barabara ya mzunguko wa nje  wa jiji la Dodoma yenye urefu wa  kilomita 112.3,  Septemba 4, 2022. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitazama sampuli za udongo wakati alipotemblea maabara ya mradi wa ujenzi  kwa kiwango cha lami wa barabara ya mzunguko wa nje  wa jiji la Dodoma yenye urefu wa kilomita  112.3.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma yenye urefu wa kilomita 112.3 ambayo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua ujenzi wake 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama makaravati wakati alipokagua mradi  wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya mzunguko wa nje  wa jiji la Dodoma yenye urefu wa kilomita 112.3  wakati alipokagua mendeleo ya ujenzi huo,  Septemba 4, 2022.  Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule na wa tatu kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatma Mganga.
 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakandarasi wa ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma kuongeza kasi ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati na kwa viwango.

 

 “Kazi inaendela vizuri, tunataka kazi ikamilike ikiwezekana hata kabla ya muda, Rais Samia Suluhu Hassan anatekeleza miradi hii ili iwanufaishe Watanzania, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunasimamia na inakamilika kwa viwango na wakati”

 

Amesema hayo leo (Jumapili, Septemba 04, 2022) wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma. Mradi huo ni sehemu ya uendelezaji wa jiji hilo.

 

Pia, Waziri Mkuu amewataka Wahandisi Wasimamizi wa mradi huo wahakikishe wanasimamia kikamilifu wakandarasi ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa viwango vilivyokubaliwa kwenye mkataba wa ujenzi wake.

 

Akizungumza na watanzania walioajiriwa katika mradi huo, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wawe walinzi wa vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi na wahakikishe vifaa vinabaki salama “Pambaneni na wote wenye nia ya kuiba vifaa hivi, tunataka tupate barabara yenye viwango”

 

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuweka utaratibu wa kuwaweka pamoja vijana ambao wanashiriki kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali nchini ili waweze kutumika zaidi kwenye makampuni ya ujenzi ya wazawa.

 

Kaimu Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Salome Kabunda amesema kuwa pamoja na mradi huo kusaidia kupunguza msongamano wa magari jiji la Dodoma pindi utakapokamilika, pia umesaidia kutoa ajira kwa wazawa zaidi ya 800.

 

“Mheshimiwa Waziri Mkuu utekelezaji wa mradi huu utawezesha kujengwa kwa vituo vya afya vinne katika mitaa ya Mahomanyika, Veyula, Nala na Ihumwa. Pia yatanunuliwa magari ya wagonjwa manne katika vituo hivyo”.

 

Aliongeza kuwa sehemu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo kutoka Nala-Veyula-Mtumba hadi bandari kavu ya Ihumwa (Km 52.5) unaojengwa kwa muda wa miezi 39, utagharimu shilingi bilioni 100.


“Sehemu ya pili ya ujenzi wa barabara hii kutoka Bandari kavu ya Ihumwa-Matumbulu hadi Nala (Km 60) unaojengwa kwa muda wa miezi 43, utagharimu shilingi bilioni 120.8 ”

 

Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilimota 112.3 unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)

 

 (mwisho)

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI SEPTEMBA 04, 2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.