Habari za Punde

Serikali inaangalia namna ya kupata wawekezaji kuwekeza kupitia nishati ya umeme wa jua (solar), nguvu za upepo na vyanzo vingine.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Balozi wa Sweden Nchini Tanzania Mhe. Charlotta Ozaki Macias, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 3-11-2022

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi ameiomba Serikali ya Sweden kushajihisha wawekezaji wa nchi hiyo kuja nchini kuwekeza katika sekta za Nishati ya Umeme pamoja na Utalii, ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuinua uchumi wake.

Dk. Mwinyi ametoa rai hiyo Ikulu zanzibar, alipozungumza na Balozi wa Sweden nchini Tanzania Charlotta Ozaki, aliyefika kwa ajili ya kujitambulisha.

Amesema katika juhudi za kuinua uchumi, Zanzibar inakabiliwa na changamoto ya umeme wa uhakika kwa vile haina vyanzo vyake binafsi vya nishati hiyo, hivyo kulazimika kutegemea huduma hiyo kutoka Tanzania Bara, huku mahitaji ya huduma hiyo yakiongezeka kutokana na kuwepo kwa shughuli nyingi za kiuchumi, ikiwemo uwekezaji katika sekta mbali mbali.

Alisema hivi sasa Serikali inaangalia namna ya kupata wawekezaji kuwekeza kupitia nishati ya umeme wa jua (solar), nguvu za upepo na vyanzo vingine.

Aidha, alisema Zanzibar imekuwa na ongezeko kubwa la ujio wa wataalii  wanaokuja nchini kila mwaka, jambo linaloifanya kuwa na mahitaji ya hoteli kubwa za kisasa pamoja na maeneo ya mapumziko.

Rais Dk. Mwinyi amemueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar imeipa kipaumbele sekta ya Uchumi wa Buluu katika kukuza uchumi wake, kwa kuzingatia kuwa ni eneo lenye fursa nyingi za kiuchumi pamoja na kuibua ajira.

Hata hivyo alisema Sekta za Uvuvi pamoja na kilimo cha mwani zinakabiliwa na changamoto, ikiwemo ya kiwango kidogo cha bei ya zao la mwani, hivyo akabainisha azma ya serikali ya kuona bei ya zao hilo inapanda ili kuleta tija kwa Taifa na wakulima.

Aidha, Dk. Mwinyi alisema Zanzibar inakabiliwa na tatizo la vijana wengi kukosa nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu kutokana na idadi ndogo ya vyuo vikuu viliopo sasa. Alisema ili kutatua changamoto hiyo, vinahitajika vyuo vingi vya mafunzo ya amali vitakavyowezesha vijana wengi waliokosa nafasi ya vyuo vikuu kujiunga na kupatiwa mafunzo mbalimbali yatakayowasaidia kuendesha maisha yao. Dk. Mwinyi alisema Zanzibar pia ina mahitaji ya kupatiwa mafunzo kwa walimu wake wa elimu ya msingi na sekondari.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Mwinyi alishukuru hatua ya mashirika na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka nchi za Umoja wa Ulaya (EU) kuunga mkono juhudi za Zanzibar kuwaletea wananchi wake maendeleo baada ya kumalizika Uchaguzi wa Mkuu wa Oktoba 2020 na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU), hivyo akaomba hali hiyo iendelee.

Alitumia fursa hiyo kuipongeza Sweden kwa misaada mbalimbali ya kiuchumi na kijamii inayoipatia Zanzibar katika sekta mbalimbali.

Naye, Balozi wa Sweden nchini Tanzania Charlotta Ozaki aliipongeza Zanzibar kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika kukuza demokrasia na na kuheshimu misingi ya haki za binadamu. Balozi Ozat alimhakikishia Rais Mwinyi kuwa Sweden itaendelea kudumisha   ushirikiano mzuri wa muda mrefu katika nyanja mbalimbali uliopo kati ya nchi yake na Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.