Habari za Punde

Uwekaji wa Fedha za Serikali BOT Kunachochea Huduma Jumuishi

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb)

Na. Haika Mamuya, WFM, Dodoma

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande, amesema kuwa Utaratibu wa sasa wa Serikali na taasisi zake kutunza fedha Benki Kuu ni mzuri na wa wazi zaidi kwa kuwa unachochea ukuaji wa huduma jumuishi za kifedha.

Hayo yamebainishwa bungeni, jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Same Magharibi, Mhe. Dk. David Mathayo David, aliyetaka kujua ni lini Benki Kuu itaweka utaratibu mzuri wa Serikali na Taasisi zake kuweka fedha katika Benki za biashara ili ilikuwa na mzunguko mzuri wa fedha

Mhe. Chande alisema kuwa, mfumo wa sasa unaiwezesha Serikali kusimamia kwa ufanisi utulivu wa uchumi jumla, hususani sarafu ya nchi na mfumuko wa bei nchini ambao ni msingi wa ukuaji endelevu wa uchumi jumuishi.

“Utaratibu wa sasa wa Serikali na taasisi zake kutunza fedha Benki Kuu unatelekezwa kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, SURA 197, alieleza Mhe. Chande.

Akijibu swali kuhusu ni lini benki kuu itashusha riba zake inapokopa kupitia hati fungani angalau kufikia asilimia 10 ili wananchi waweke fedha zao kwenye benki za biashara, Mhe. Chande alisema kuwa riba zinazopatikana kwenye dhamana za Serikali ikijumuisha Hatifungani hazitolewi au kuwekwa na Benki Kuu ya Tanzania bali matokeo ya mchakato wa mauzo na ununuzi wa dhamana na hatifungani katika soko la fedha.

Aliongeza kuwa riba katika soko huamuliwa na ujazi na utashi wa dhamana hizo za Serikali (supply and demand) katika soko la fedha linaloendeshwa kwa mfumo wa soko huria.

Mhe. Chande ameeleza kuwa takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa riba za hatifungani zinaendelea kupungua kutoka wastani wa asilimia 8.52 hadi 16.71 mwaka 2017/18 na kufikia asilimia 4.4 hadi 13.61 mwaka 2021/22.

Alisema kuwa kwa upande wa riba za mikopo, zimepungua na kufikia wastani wa asilimia 16.41 mwaka2021/22 kutoka asilimia 17.86 mwaka 2017/18.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.