Habari za Punde

Umuhimu wa Kuanzishwa kwa Madawati ya Jinsia Ndani ya Vyuo Vikuu Ili Iwe Suluhisho -Waziri Pembe

Na Maulid Yussuf WMJJWW.Zanzibar.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe.Riziki Pembe Juma amesema Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wanakumbana na changamoto mbalimbali za Udhalilishaji na ukatili wa kijinsia wakiwa Vyuoni.

Amesema kutokana na hali hiyo Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Wizara ya maendeleo ya Jamii Jinsia na Makundi Maalumu  zimeona umuhimu wa kuanzishwa kwa madawati ya Jinsia ndani ya Vyuo Vikuu Tanzania ili iwe suluhisho la changamoto hiyo vyuoni.

Akizungumza wakati wa akizindua Dawati la Jinsia la Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU)  katika Ukumbi wa Chuo hicho Kibele, Mhe Riziki amesema tafiti mbalimbali zimefanywa ambazo matokeo yake yameonesha kuwepo kwa changamoto hiyo katika vyuo.

Amesema kwa vile suala la Elimu ya juu ni suala la Muungano, Vyuo Vikuu vya Zanzibar pia vinalazimika kutimiza jukumu hili kwa mujibu wa muongozo uliozinduliwa na Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaaliwa ambapo vyuo vyote vya Tanzania viwe vimefungua Dawati hilo ifikapo Disemba 30 mwaka huu.

Mhe Riziki amewataka viongozi wa ZU kuhakikisha wanafuata muongozo uliowekwa katika kuhakikisha dawati hilo linakuwepo na linafanya kazi  kama ilivyoelekezwa.

Pia amesema, kuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu ni heshima na hadhi kubwa sana kitaaluma na kijamii na haipendezi kwa Mhadhiri au mfanyakazi kutumia nafasi aliyo nayo kwa ajili ya kuwafanyia ukatili Wanafunzi wao.

" Haipendezi haipendezi, haipendezi kwa wahadhiri badala ya kufanya kazi zao za utafiti wanajihusisha na vitendo vya udhalilishaji, Serikali hatutamuacha, tutaenda nae sambamba,  amesisitiza Mhe Riziki. 

Aidha amewataka Wanafunzi wa ZU kuhakikisha wanalitumia vyema dawati hilo kwa kutoa taarifa atakaepata tatizo la udhalilishaji wa aina yeyote, na si kwa kumsingizia mwalimu kwani haitakuwa jambo jema.

Naye Naibu Kaimu Makamu Miuu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar ZU na Mkuu wa Kitivo cha Sheria, Dk Yahya Khamis Hamad amesema ZU ipo pamoja na Serikali katika kushughulikia masuala ya Elimu lakini bado kuna changamoto katika kuwepo kwa usawa wa kijinsia.

Kwa kuona umuhimu wa hilo ZU imejidhatiti katika kuhakikisha inashirikiana na serikali katika kusimamia suala hilo.

Kwa upande wake Mlezi wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar ZU,  bwana Juma Rashid khamis amewataka Wanafunzi kujitambua na kujiamini katika masomo yao pamoja na kuhakikisha wanaweka mipaka kati yao na Walimu wa wanawake na wanaume  ili kuepukana na vitendo vya udhalilishaji chuoni hapo.

Amesema ni lazima wanaume kusimama imara na kujua kuwa wao ni wasimamizi wa wanawake kama aya za qur-aan inavyoleza, hivyo ni vyema kuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya wanawake kwa kuzingatia misingi ya dini ili kuwa na maisha bora.

Pia amewataka kuhakikisha kila mwenye malalamiko yake kuyafikisha katika dawati hilo ili kuweza kupatiwa ufumbuzi na chuo hicho kiwe mfano katika kusimamia haki na usawa katika masuala ya jinsia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.