Habari za Punde

Wajasiriamali wadogo wadogo washiriki maonyesho ya EAC Kampala Uganda

 NA MAULID YUSSUF WMJJWW. Kampala Uganda


Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Riziki Pembe Juma ametoa salamu za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika ufunguzi wa maonesho ya 22 ya wajasiriamali wadogo wadogo na wa kati,nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki EAC,  yanayoendelea katika viwanja vya Jamuhuri KOLOLO, Kampala Uganda.


Akitoa salamu hizo kwa niaba ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na watanzania wote, Mhe Riziki ameishukuru Jamuhuri ya Uganda kwa umoja na ushirikiano wao kwa wajasiriamali na maafisa kutoka Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema katika maonesho  hayo jumla ya 
Wajasiriamali 250 kutoka Tanzania wameshiriki kuonesha na kuuza bidhaa zao ambapo kati yao asilimia 87 ni wanawake.

Amesema hali hiyo inaonesha kuwa uongozi wa Dkt, Samia Suluhu Hassan unatoa kipaumbele kwa wanawake kwa kuzingatia kuwa mwanamke ni kiungo thabiti katika maendeleo ya familia na nchi kwa ujumla.

Pia amesema katika maendeleo, ushirikiano wa jinsi zote umekuwa ukijenga uchumi usiotetereka na Maendeleo mazuri kwa wajasiriamali. 

Hivyo amesema wamekuwa wakishuhudia ongezeko la ubora wa bidhaa za wajasiriamali hao kila mwaka ikiwa ni dalili kubwa ya kuwa lengo la maonesho hayo limefikiwa kutokana na wajasiriamali hao hufika kwa  kujifunza, kubadilishana uzoefu wa kiteknolojia kutoka kwa wajasiriamali wa ndani na nje ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Hata hivyo amesema Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na ndugu zao wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kufikia malengo yake iliyojiwekea.

Naye Mwenyekiti Mkazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, bwana Josephat Rweyemamu amesema wakati Mataifa mbali mbali yakizungumzia masuala ya uchumi wa Buluu, Zanzibar ni miongoni mwa nchi iliyopiga hatua kubwa katika uchumi wa buluu kati ya nchi wanacha wa Afrika Mashariki.

Bwana Josephat ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa juhudi hizo na kuiomba kuendelea ili kuweza kukuza uchumi wake.

Maonesho hayo ya wajasiriamali wadogo wadogo na wa kati yamekuwa yakifanyika kila mwaka katika nchi wanachama wa Afrika Mashariki, yameanza tarehe 8 Disemba na  yanatarajiwa kumalizika tarehe 18 disemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.