Habari za Punde

Waziri wa Mambo ya ndani akutana na kufanya mazungumzo na Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na usalama, Ziwani

Na Ali Issa Maelezo, 30/12/2022

WAZIRI wa Mambo ya ndani wa Tanzania, Injinia Hamadi Yussuf Masauni amesema ushirikiano wa vyombo vya ulinzi na usalama ni njia mojawapo ya kuimarisha ulinzi nchini.

Hayo ameyasema huko Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar, Ziwani wakati alipokuwa akizungumza na Wakuu wa Vikosi mbali mbali vya Ulinzi na usalama .

Amesema ushirikiano wa pamoja katika utekelezaji wa kazi utasaidia kuimarisha amani na utulivu nchini na ndio njia pekee kuleta matumaini makubwa kwa wananchi.

Amesema kuwa iwapo vikosi vitashirikiana kwa pamoja katika utekelezaji wa majukumu yao  kutasaidia kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuvibaini vigenge vya wahalifu.

“Ikiwa wahalifu wanashirikiana katika uovu kwanini na sisi tusishirikiane katika kuleta usalama ulio imara na usio tetereka ni jambo tulitumieni”,alisema Waziri Masauni

Aidha alifahamisha kuwa kwa sasa hali ya Amani Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla inaridhisha ijapo kuwa zipo tafrani ndogo ndogo ambazo haziwafanyi wananchi kusita kufanya kazi zao za kujiletea Maendeleo.

Alisema hivi sasa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kumekuwa na suala kubwa la uwekezaji kwa wageni na Wazawa kwa hivyo ipo haja kubwa vikosi hivyo kuwa pamoja katika utekelezaji wa majukumu yao kufanya hivyo kutasaidia kufanikisha azma ya Serikali ya  kuhakikisha kuwepo na usalama wa ulinzi wa watu na malizao.

Alieleza kuwa Makatibu Wakuu wa Wizara za Vikosi vya Ulinzi na usalama kuwataka kulichukulia hatua ili kuona hali hiyo inaenda kwa utaratibu uliopangwa.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Hamza Hassani Juma alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  inasisitiza ushirikiano wa vikosi vyote pamoja na wananchi ili kuona Zanzibar iko salama jambo ambalo litaimarisha hali ya Amani na utulivu nchini  .

Amesema  kuwa hivisasa Tanzania imekuwa ikipokea watalii wengi zaidi hivyo ushirikiano wa ulinzi na usalama kwa wageni kutasaidia kuzuia uhalifu kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla .

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Idara Maalum za SMZ Masoud Ali Muhamed amesema suala la ulinzi na usalama katika nchi ni jambo la lazima hivyo vikosi vyake vitakuwa tayari kutoa ushirikiano na kuwa mstari wa mbele katika kulisimamia hilo.

Alisema ushirikiano huo ni jambo jema kwani lengo kuu la kuwepo vikosi vya ulinzi na usalama ni kuhakikisha kuwa kuna amani ya kudumu.

Kikao hicho kiliwashirikisha viongozi wa vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini Tanzania wakiwemo Mawaziri,Makamishna pamoja na Viongozi mbali mbali  wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa Idara Malumu SMZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.