Habari za Punde

Mhe Hemed atembelea Maonesho ya Tisa Biashara ya Biashara viwanja vya Maisara
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameipongeza Wizara ya Biashara na maendeleo ya viwanda kwa kuboresha  Maonesho ya Tisa Biashara ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Maisara Mjini Zanzibar.

Mhe. Hemed ameyasema hayo alipotembelea Maonesho hayo kujionea shughuli zinazofanywa na washiriki mbali mbali wa monesho hayo.

Amesema maonesho hayo ni ya aina yake hasa kuona washiriki wa  Zanzibar na nchi mbali mbali ambapo kuongezeka kwa ushiriki wao kuonesha kuwepo kwa maandalizi mazuri yanayosimamiwa na Wizara ya Biashara na maendeleo ya viwanda.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Maonesho hayo yanawapa fursa wananchi kupata huduma mbali mbali katika eneo moja tu ambazo ilikuwa wazifate  masafa marefu.

Aidha Mhe. Hemed amewataka Wananchi kujitokeza na kutembelea Taasisi za Serikali zinazotoa huduma pamoja na kupata maelekezo kuhusiana na huduma wanazozitoa.

Aidha Mhe. Hemed amefurahishwa kuwepo kwa kituo jumuishi (One Stop Center) katika Maonesho hayo ambacho kinajumuisha Taasisi mbali mbali zilizoshiriki na kueleza kuwa uwepo wa Kituo hicho kunaonesha ushirikiano uliopo baina ya Taasisi mbali mbali.

Nae waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe. Omar Said Shaban amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kutembelea maonesho hayo jambo ambalo linawatia hamasa   Wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea maonesho hayo.

Aidha Mhe. Shaban amemuhakikishia Mhe. Hemed kuwa Wizara itaendelea kuchukua maelekezo watakayopatiwa na Viongozi mbali mbali wanaokuja kutembelea kwa lengo la kuboresha maeonesho hayo.

Akitembelea maonesho hayo Mhe. Hemed amezishauri Taasisi zinazotoa huduma kwa wananchi  kuboresha huduma zao hasa kutumia muda mfupi kuwapatia huduma wanazostahiki.

Katika Maonesho hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa kuisalimia timu ya Mpira wa Nage ya Fufuni Wilaya ya Mkoani ambayo inashiriki Mashindano ya Nage ya  Mapinduzi ambapo amewapongeza kwa hatua waliofikia ya Nusu Fainali na kuwataka kuzingatia nidhamu katika michezo.

 

……………………………..

Abdulrahim Khamis

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.