Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amejumuika na waumini wa Masjid Utapoa Bububu Wilaya ya Magharibi “A” katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.
Akiwasalimia waumini hao baada ya Swala Alhajj Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi inachukua jitihada mbali mbali katika kuleta unafuu wa bei za bidhaa ili wananchi waweze kujikimu kimaisha.
Amesema pamoja na jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wapo baadhi ya wafanyabiasha wanapandisha bei za bidhaa bila ya kuwa na sababu za msingi jambo ambalo wanaenda kinyume na jitihada za Serikali za kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi wake.
Pamoja na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewakumbusha waumini hao kuwa na tabia ya kupendana na kusaidiana kwa kuwajali watu wenye mahitaji maalumu katika jamii wakiwemo mayatima,watu wenye ulemavu pamoja na wajane.
Aidha Alhajj Hemed amewahimiza waumini na wananchi kwa ujumla kuendelea kuitunza amani iliyopo ili Serikali iendelee kuwatumikia wananchi wake na kuwaletea maendeleo.
Pamoja na hayo Mhe. Hemed amewakumbusha waumini hao kusimamia misingi ya dini katika maisha yao ya kila siku na kudumisha ibada hasa katika miezi hii mitukufu ili kupata radhi za Allah (S.W.)
Nae Maalim Omar Hamad ameiomba Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kusimamia mila,silka na desturi ili kuepusha mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Ameeleza kuwa katika Jamii kumeibuka mambo mbali mbali yanayoashiria kupotea kwa maadili ya wazanzibari hali ambayo inapaswa kukemewa kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo
No comments:
Post a Comment