Habari za Punde

Ujenzi wa msikiti mpya wa Masjid Fatma Kilimani umesadifu mipango ya Serikali ya kubadili mandhari ya mji wa Zanzibar

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Wananchi baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa na ufunguzi wa Masjid Fatma Ahmad Merdas Kilimani Wilaya ya Mjini Unguja uliofunguliwa leo 10-2-2023 kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid hiyo

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ujenzi wa msikiti mpya wa Masjid Fatma Kilimani umesadifu mipango ya Serikali ya kubadili mandhari ya mji wa Zanzibar kuwa wa kisasa kwa kubadili hali halisi ya eneo hilo.

Al hajj Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati akifungua msikiti huo uliopo Kilimani Wilaya ya Mjini Magharibi, alikotekeleza ibada ya sala ya Ijumaa.

Alisema Serikali ya awamu ya nane inampango wa kutoa mji mpya kwenye eneo lililojengwa msikiti huo na kueleza ujenzi wake umeakisi adhma ya Serikali ya kubadili taaswira ya mandhari ya eneo la Kilimani kuwa na haiba ya mji wa kisasa.

“Ni kweli eneo hili limo kwenye mpango mpya wa Serikali wa kubadili mandhari ya zamani kuwa ya kisasa pamoja na mipango mipya wa Serikali, imeona lazima kuwe na misikiti kwa sharti la msikti mzuri na wa kisasa, leo nafarajika sana kuwa matarajio yangu ya Kilimani kuwepo na msikiti wa kisasa yametimia”, Alisifu Al hajj Mwinyi.

Akizizungumzia nyumba za Maendeleo za Kilimani  zilizopo jirani na msikiti huo, Al hajj Dk. Mwinyi alieleza kwamba zilijengwa miaka mingi iliyopita na kwamba hatua ya awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuzifanyia mabadiliko makubwa kwa kubadili haiba na mwonekano halisi wa eneo hilo kuwa mji wa wakisasa wenye kumvutia na kumpendezesha kila mtu anaetembelea mji wa Zanzibar.

Aidha, Al Hajj Dk. Mwinyi aliwashukuru wafadhili wa masjid Fatma kwa ujenzi wa msikiti mzuri, mkubwa na wakisasa katika eneo hilo.

Alieleza kufarajika kwake kuona mabadiliko na ujenzi wa misikiti mipya na ya kisasa katika kila eneo la Zanzibar, mijini na Mashamba.

Al Hajj Dk. Mwinyi aliwaomba wafadhadhili kuendelea kuisaidia Zanzibar kwa kuijengea misiti mingi mikubwa na yenye ubora ambayo itabadili madhari ya miji na kuwa sehemu salama kwa waumini kuendelea kufanya ibada.

Akizungumzia suala la maegesho ya magari na bustani nzuri itakayopendezesha mandhari ya msikiti huo, Al hajj Dk. Mwinyi alisema Serikali imetoa kibali cha kuendelea na ujenzi ambao alieleza utatekelezwa na mfadhili wa msikiti huo. Pia Al hajj Dk. Mwinyi alisema Serikali itatoa eneo mahala hapo kujengwe hospitali kubwa ya macho itakayosadifu hali halisi ya mwonekano mpya wa mji ambayo itawahudumia wananchi wote wa Zanzibar.

Alisema msikiti uko eneo karibu na barabara kuu hivyo, itakua vigumu kwa magari kupata eneo la maegesho, alieleza Serikali kupitia Shirika la nyumba la Zanzibar wako tayari kutoa eneo hilo.

Hata hivyo, aliwataka waumini kuendelea kuitunza misikiti na kuiendeleza endapo itapatwa na hitilafu kwa kuitengeneza.

Akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa msikiti huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman aliishukuru Serikali kwa kukubali kutoa eneo hilo kujengwa msikiti mkubwa na wakisasa.

Mapema akitoa nasaha za Ijumaa kwa waumini waliofika kutekeleza ibada ya sala msikitini hapo, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Khalid Ali Mfaume aliwataka waumini waeneo hilo kuimarisha misikiti kwa kuiboreshea usafi na mwonekano wake pamoja kukarabati itakapochakaa au kuharibika. Aidha, aliwaeleza waumini na uongozi wa msikiti huo kuendelea kutoa taaluma zenye kujenga na kutengeneza jamii zilizo bora.

Akihutubu msikitini hapo, Ust. Abdalla Zubeir Maruzuku ambae pia aliongoza sala hiyo alisema suala la ujenzi wa msikiti linahitaji imani ya dhati ya dini kwani malipo na fadhila zake ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Alisema sala ni ibada kuu kwenye misikiti ambayo inahusisha sifa za daraja kubwa tatu za Mwenyezi Mungu kwa atakae simamisha kwa dhati ya imani yake na kutoa zaka.

Awali akisoma risala ya kwa niaba ya uongozi wa msikiti huo, Kaadhi wa Mahakama ya Wilaya, Ust. Hemed Saleh Mbarouk, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane kwa ushirikiano walioutoa tokea hatua za awali hadi kukamilika kwa ujenzi wa msikiti huo.

Masjid Fatma kwa mara ya kwanza ulijengwa mwaka 1951 chini ya uongozi wa  Imamu wa kwanza Marehemu Skeikh Yussuf Mshamba Ngwali, wakati huo uliitwa, Msikiti wa Kiinuamiguu, baadae mwaka 1970 ulivunjwa na Serikali ya awamu ya kwanza ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Marehemu Mzee Abeid Aman Karume, baada ya kujengwa mji wa wakati huo.

 Aidha, ufunguzi wa msikiti huo wa kisasa ulihudhuriwa pia na Marais wastaafu awamu ya sita na ya saba, Alhajj Dk. Aman Abeid Karume na Al Hajj Dk. Ali Muhamed Shein, Spika wa baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Omar Saleh Kaab, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana pamoja na Mashikh na Maimamu na wafadhili wa msikiti huo.

IDARA YAMAWASILIANO – IKULU, ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.