Habari za Punde

Katibi Mkuu Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Amali Zanzibar Ndg.Khamis : Asisitiza Ubunifu Kiutendaji

KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdulla Said,akizungumza na Watendaji wa Idara ya Elimu Mbadala na Elimu ya Watu Wazima katika Wizara hiyo Mazizini Unguja.

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdulla Said,amewasihi Watendaji wa idara na vitengo vya Wizara hiyo kujitathimini kiutendaji na badala yake watekeleze wajibu wao na kuongeza ubunifu kiutendaji.

Nasaha hizo amezitoa wakati akizungumza na watendaji wa idara ya Elimu ya Mbadala na Watu Wazima pamoja na Bodi ya Mikopo Zanzibar, huko katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo Mazizini Zanzibar.

Khamis,alisema Wizara hiyo ni uti wa mgongo wa maendeleo ya nchini kwani ina dhamana ya kusimamia uzalishaji na upatikanaji wa wataalamu wenye uwezo na waliobobea katika fani mbalimbali nchini.

Alieleza kuwa ni lazima watendaji hao wawe mfano wa kuingwa katika masuala ya utendaji,nidhamu,kujituma na ubunifu katika sehemu zao za kazi ili kwenda sambamba na kasi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk,Hussein Ali Mwinyi kiutendaji.

Katika maelezo yake Katibu Mkuu huyo Khamis, alisema kupitia Wizara hiyo wanasimamia upatikanaji wa huduma bora za kielimu pamoja na mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wote wenye vigezo ili wasome bila vikwazo.

Alifafanua kwamba muelekeo na mstakabali wa maendeleo endelevu ya nchi unaanza kupimwa kutoka katika taasisi zinazosimamia uzalishaji wa wataalamu watakaotafsiri kwa vitendo sera,dira na mipango ya maendeleo ya nchini iwafikie kwa haraka wananchi wa mijini na vijijini.

“Watendaji wenzangu hivi ni vikao vyangu vya mwanzo toka nilipoteuliwa kutumikia nafasi hii ya Katibu Mkuu,dhamira yangu ni kuondoa vikwazo na urasimu ili tufanye kazi kwa pamoja na twende na kasi ya kimtandao ya 5G katika wajibikaji wetu wa kila siku.  

Najua tunakabiliwa na changamoto mbalimbali lakini zisiwe vikwazo vya kukwamisha kazi zilizokuwa ndani ya uwezo wetu kiutendaji, nitaendelea kufanya juhudi za kutatua changamoto hizo kidogo kidogo huku tukichapa kazi.”, alieleza Katibu Mkuu huyo Khamis.

Pamoja na hayo aliwakumbusha watendaji hao kuhakikisha kazi zao zinaendana na malengo ya Mkataba wa Serikali na Wananchi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025, inayoelekeza Wizara hiyo utekeleza kwa ufanisi majukumu yake.

Sambamba na hayo aliwapongeza watumishi wote wa Wizara hiyo kwa juhudi zao katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali, na kuongeza kuwa mafanikio na heshima ya taasisi hiyo itaendelea kujengwa na watendaji hao.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Mbadala na Elimu ya Watu Wazima Mashavu Ahmada Fakih,alisema atayafanyia kazi kwa vitendo maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu huyo.

Kwa upande wao baadhi ya watendaji hao wameeleza kuwa wanakabiliwa na changamoto za upungufu wa vitendea kazi zikiwemo komputa,usafiri na fedha za kujikimu panapotokea kazi za dharura katika maeneo ya vijijini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.