Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt.
Switbert Mkama wakati akifungua Warsha ya siku mbili ya kujadili Matokeo ya
Mkutano wa 27 na Maandalizi ya Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa
Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi leo Mei 11, 2023 jijini Dodoma.
Washiriki wakiwa katika Warsha ya siku mbili ya kujadili
Matokeo ya Mkutano wa 27 na Maandalizi ya Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa
Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi leo Mei 11, 2023 jijini Dodoma.
Fursa hiyo
imekuja kutokana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kuwakutanisha Marais watano kutoka Zambia, Zimbabwe, Malawi, Botswana,
Makamu wa Rais wa Angola na watendaji kutoka Benki ya Dunia na Benki ya
Maendeleo ya Afrika katika uzinduzi wa mtandao wa uzalishaji wa pamoja wa
nishati jadidifu kwa nchi za kusini mwa Afrika na kujadili fursa za uwekezaji
katika sekta hiyo na miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Hayo
yamebainishwa leo Mei 11, 2023 jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya
Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama wakati akifungua Warsha ya Kujadili Matokeo
ya Mkutano wa 27 na Maandalizi ya Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa
Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.
Amesema kuwa miradi
hiyo itafadhiliwa na Benki ya Dunia, Taasisi ya Afrika 50 na Shirika la Nishati
la Afrika kwa kushirikiana na kampuni ya China Renewable Energies ambapo Kampuni
ya Equinor iliahidi kukamilisha makubaliano ya mkataba wa ufadhili wa
mradi wa gesi ifikapo Disemba 08, 2022.
Akiendelea
kutaja mafanikio ya mkutano huo, Dkt. Mkama amesema Kampuni ya TAQA ARABIA ya
Misri imeahidi kujenga vituo 12 vya kusambaza gesi asilia kuanzia mwaka 2023
pamoja na kujenga uwezo wa vijana kuhusu teknolojia ya gesi katika vyombo vya
usafiri.
“Mtakumbuka
katika Mkutano wa COP 27 Tanzania ilikuwa na banda lake ambalo uwepo wake umetoa
fursa kubwa kwa Tanzania kujulikana na kupatikana kirahisi wakati wa mikutano
ikiendelea. Hali ambayo iliwezesha kufanya majadiliano na kutoa ufafanuzi
kuhusu fursa za uwekezaji na ushirikiano na vipaumbele vya nchi kuhusu hifadhi
na usimamizi wa mazingira,“ amesema.
Kaimu Katibu
Mkuu ameongeza kuwa Shirika la The Nature Conservancy (TNC) lipo tayari
kuisaidia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika kuanza biashara ya kuuza Hatifungani za Bluu (Blue Bond).
Itakumbukwa kuwa
Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika na programu ya uchumi wa bluu na
kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika bara la Afrika inayofadhiliwa na Benki
ya Dunia. Serikali ya Norway imeahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika
masuala ya mabadiliko ya tabianchi, hususan utekelezaji wa Mchango wa Taifa wa Kukabiliana
na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC).
Mkutano wa 27 ulifanyika Sharm El
Sheikh nchini Misri na Mkutano wa 28 unatarajiwa kufanyika Novemba 30 hadi 12
Disemba 2023 jijini Dubai katika, Muungano wa Falme za Kiarabu.
No comments:
Post a Comment