Habari za Punde

UVCCM ZANZIBAR : Yasema Italinda Maslahi ya CCM kwa Gharama Yoyote

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Zanzibar,umempongeza Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Mwinyi, kwa dhamira yake ya kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana waliojitolea kwa muda mrefu ndani ya Chama na Jumuiya hiyo.  

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar  Ndg.Mussa Haji Mussa, alipozungumza na mwandishi maalum huko Afisi kwake Gymkhana Unguja, alisema umoja  huo utaendelea kuenzi,kuthamini,kulinda na kupigania kwa gharama yoyote maslahi ya CCM.

Alieleza kuwa maamuzi hayo ya Dk.Mwinyi, yanatokana na utekelezaji wa mipango endelevu iliyomo katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025, ibara ya 136 kifungu kidogo ( C) kinachoelekeza kuwa ifikapo mwaka 2025 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itazalisha zaidi ya ajira 300,000 katika sekta rasmi na zisizo rasmi.

Mussa, alisema kitendo cha Makamu Mwenyekiti huyo Dk.Mwinyi, kuwaahidi vijana kwamba atawapa kipaumbele katika mchakato wa ajira ni maamuzi sahihi yanayotakiwa kupongezwa na kuungwa mkono na vijana wote wa Zanzibar.

Alieleza kuwa UVCCM Zanzibar imekuwa Jumuiya imara inayozalisha viongozi makini,wazalendo,waadilifu na wenye misimamo isiyoyumba katika kulinda maslahi ya watu na nchi kwa ujumla.

Alisema ziara ya kichama ya Makamu huyo Mwenyekiti imekuwa ni chachu ya kuongeza ari,hamasa,uzalendo na utii wa kiwango cha juu kwa vijana wote waliolelewa katika misingi ya itikadi na sera za CCM nchini.

“Tunampongeza kwa dhati Makamu Mwenyekiti wetu wa CCM Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi, na tunamuahidi kuwa tutaendelea kuwa Vijana imara,wawakamavu,wapambanaji,waadilifu na wenye maoni na fikra za kuenzi na kukitumikia Chama na Jumuiya ya UVCCM  usiku na mchana.

Pia tutaendelea kufanya kazi za ujenzi wa taifa kwa bidii kubwa na kwa dhamira na falsafa ya kuenzi waasisi wetu na vyama vya ASP na TANU” ,aliseahidi Naibu Katibu Mkuu huyo.

Katika maelezo yake Naibu Katibu Mussa, alimshukru Dk.Mwinyi kwa kupokea,kushauri na kuelekeza masuala mbalimbali ya kiutendaji katika ziara yake ya kutembelea miradi miwili mikubwa ya kimkakati ya UVCCM Zanzibar.

Pamoja na hayo Mussa, alieleza kuwa UVCCM inarithishwa na kazi kubwa ya kiutendaji ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Mwinyi, hasa kupitia maelekezo na mipango endelevu aliyoitoa katika ziara yake ya Kichama Mkoa wa Mjini Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.