Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameutaka uongozi wa Benki ya NMB kuendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika nyanja mbali mbali za kijamii.
Akizungumza katika hafla ya Chakula cha jioni ya kuadhimisha kutimia miaka ishirini na tano (25) ya Benki ya NMB iliyofanyika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege amesema benki hiyo imekuwa ikitoa msukumo mkubwa katika kuendeleza utalii wa Zanzibar ambapo kwa mwaka huu imesaini mkataba wa kuhifadhi bustani ya forodhani ambayo inatembelewa na watalii kutoka nchi mbali mbali.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Benki hiyo inatoa ushirikiano kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuboresha mifumo ya huduma za kidigitali ndani ya Serikali pamoja na kuwapatia ajira Vijana.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameipongeza NMB kwa kutenga gawio kwa masuala ya kijamii ambapo katika hafla hiyo amekabidhiwa mfano wa Madawati Mia Nne na Saba 407 yaliyogharamia Millioni Arobaini na Tatu (43,000,000) ambapo yatagaiwa kwa Skuli Tatu za Zanzibar pamoja na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume.
Mhe. Hemed ameto wito kwa Benki ya NMB kuendelea kusaidia katika sekta mbali mbali ikiwemo uvuvi, utalii na kilimo ambapo amezitaka Taasisi nyengine zinazotoa huduma za kifedha kujifunza kupitia Benki hiyo ambapo hufanya kazi kwa ukaribu na Serikali na jamii jambo linalotoa tija kwa Taasisi zao na Serikali kwa ujumla.
Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruthi Zaipuna amemueleza Mhe. Hemed kuwa Benki hiyo inafanya kazi kwa ushirikiano na Mamlaka za Seriklai mtandao kwa njia ya kielektroniki, kuhifadhi Mapato na kufanya malipo kwa haraka Zaidi kupitia mfumo huo.
Amesema NMB itaendelea kuunga Mkono mipango mikakati ya Serikali katika kuwaletea Wananchi maendeleo kwa kuboresha mauzo na kurejesha faida katika jamii kwa kutoa misaada mbali mbali.
Sambamba na hayo Bi Ruthi amesema Benki ya NMB imedhamiria kupanda miti Zaidi ya Milioni moja kwa nchi nzima kwa lengo la kutunza na kuhifadhi mazingira na kuendeleza ushirikiano kwa jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya NMB Dkr. Edwin Mhede amemuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Benki ya NMB itaendelea kulipa stahiki kwa wakati pamoja na kuipatia Serikali gawio la faida litokanalo na huduma wanazozitoa ambapo kwa mwaka huu gawio limeongezeka maradufu kulinganisha na nyakati zilizopita kutokana na mpango wao wa kutanua wigo mpana wa kibiashara na huduma za jamii.
Katika hafla hiyo Mhe. Hemed amekabidhi zawadi mbali mbali kwa washindi wa Bonanza la Michezo mbali mbali lililoandaliwa na Benki hiyo lilifanyika katika Viwanja vya Mao Ztung.
Kutimiza Miaka Ishirini na Tano (25) kwa Benki ya NMB kunatanua wigo wa kibiashara ikiwa na Matawi Zaidi ya Mia Mbili Ishirini na Nane (228), Mawakala Elfu Ishirini (20,000,000) kwa Zanzibar hadi sasa wana Matawi Matatu (03) na wamedhamiria kufungua Matawi mengine Matatu (03) ili kuweza kusogeza huduma zao karibu na Wananchi hasa kwa Watalii wanaoingia Nchini.
No comments:
Post a Comment