Habari za Punde

Mkakati wa SMZ wa Kuwarejesha Skuli Watoto Walioacha Masomo Zanzibar

MRATIBU wa mradi wa kuwarejesha watoto Skuli Zanzibar Mzee Shiraz Hassan, wakati akifungua kikao kazi cha kujadiliana mbinu bora za kuwarejesha watoto skuli walioacha masomo cha Wenyeviti wa Kamati za Skuli na Polisi Jamii wa Wilaya za Magharibi ‘’A’’ na Magharibi “B”, kilichofanyika  Skuli ya Sekondari ya Aboud Jumbe Mwinyi iliyopo Fuoni Zanzibar.
BAADHI ya Wenyeviti wa Kamati za Skuli na Wajumbe wa Vikundi Shirikishi vya Polisi Jamii wakifuatilia hotuba na maelekezo ya Mgeni rasmi ambaye ni Mratibu wa mradi wa kuwarejesha Watoto Skuli Zanzibar Mzee Shirazi Hassan, katika Kikao Kazi kilichofanyika katika Skuli ya Sekondari ya Aboud  Jumbe Mwinyi  Juni 04,mwaka 2023.

NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.

WENYEVITI wa Kamati za Skuli pamoja na Vikundi vya Ulinzi Shirikishi nchini,wameshauriwa kutoa taarifa sahihi za watoto walioacha masomo na kubaki mitaani ili warudishwe skuli na waendelee kupatiwa elimu.

Rai hiyo imetolewa na Mratibu wa mradi wa kuwarejesha watoto skuli Zanzibar Mzee Shiraz Hassan, wakati akifungua kikao kazi cha kujadili mbinu bora za kuwarejesha watoto skuli walioacha masomo kilichowashirikisha Wenyeviti wa Kamati za Skuli na Polisi Jamii wa Wilaya za Magharibi ‘’A’’ na Magharibi “B”, kilichofanyika  Skuli ya Sekondari ya Aboud Jumbe Mwinyi iliyopo Fuoni Zanzibar.

Alisema dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kuhakikisha watoto wote nchini wanapatiwa haki yao ya msingi ya elimu kwa ngazi mbalimbali ili kujenga jamii yenye watu wanaojua kusoma na kuandika sambamba na wataalamu wa fani tofauti.

Shirazi,alisema lengo la kikao hicho ni kujadiliana na Wadau hao ambao wapo karibu zaidi na jamii kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi za Wanafunzi walioacha Skuli ili Waratibu wa Elimu wa ngazi za Wilaya na Mikoa wachukue hatua za watoto hao  kuendelea  kusoma.

Mratibu huyo Shirazi, alisema jumla ya Wanafunzi 28,981 wamerejeshwa skuli kati ya wanafunzi 35,732 walioacha masomo ikiwa dhamira ya Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ni kuhakikisha Wanafunzi 6,751 waliobaki mtaani ifikapo 2024 watarudi skuli kuendelea na masomo.

“Tunaendelea kuhamasisha jamii yetu na kutoa elimu juu ya umuhimu wa watoto walioacha skuli warudishwe na kuendelea na masomo Serikali tayari inafanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha wanasoma bila vikwazo.

Pia nitoe wito kwa Walimu Wakuu wanapopelekewa wanafunzi wa aina hiyo waache urasimu wa kuweka vikwazo badala yake wafuate utaratibu uliowekwa na Serikali kwa kesi za aina hiyo ili tufikie dhamira ya Serikali ya kuhakikisha vijana na watoto wote wanapata elimu.”,alisema Shirazi.

Alieleza kuwa watoto wote wenye umri wa miaka 7-14 walioacha skuli wamewekewa mazingira rafiki ya kuendelea na masomo na kwamba wale wenye umri wa zaidi ya miaka 15 nao wamewekewa utaratibu maalum kupitia usimamizi wa Elimu Mbadala nchini.

Alisema Serikali ya awamu ya nane chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi,inaendelea na mkakati wa kuwarudisha  Skuli watoto wote huku wakisaidiwa  vifaa vikiwemo sare na madaftari na vitabu na kupewa elimu bure.  

Katika maelezo yake Mratibu huyo,aliwasihi Walimu kutambua na kutumia mbinu za dhana ya Saikolojia kubaini changamoto zinazowakabili wanafunzi ili zitafutiwe ufumbuzi wa haraka kabla mwanafunzi hajafikia uamuzi wa kuacha skuli.

Shirazi, alifafanua kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wanakuwa na changamoto za kifamilia,wenye matatizo ya ulemavu wa aina mbalimbali na wengine wanakabiliwa na msongo wa mawazo kutokana na kufanyiwa vitendo vya udhalilishwaji wa kijinsia hivyo kusababisha kuacha skuli.

Naye Mkuu wa Divisheni ya Elimu Mbadala Zanzibar Waziri Rajab Hamza, alisema Serikali inaendelea kuchukua juhudi ya kuwaridisha watoto hao skuli ili waendelee na masomo hivyo jamii inatakiwa kuunga mkomo juhudi hizo kwa kuhakikisha watoto hao hawaachi masomo na kurudi tena mtaani.

Kwa upande wao washiriki wa kikao hicho, alisema watahakikisha wanafuata maelekezo yaliyotolewa ili kukamilisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha watoto wote nchini wanapata elimu kulingana na mahitaji yao.

Aliomba Serikali kuchukua hatua kali za kuthibiti michezo ya kisasa katika vibanda vinavyoonyesha video games maarufu kama ‘Play Station’,kamari,utumiaji wa dawa za kulevya kwa baadhi ya wanafunzi sambamba na kurejeshwa kwa utaratibu wa kila mwezi wanafunzi wa kike kupimwa afya zao hasa ujauzito.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.