SERIKALI ya Mapinduzi
ya Zanzibar imesema itawachukulia hatua za kisheria watumishi kutoka taasisi na
mashirika ya Umma walioshindwa kutoa majibu kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti ya mwaka wa Fedha 2022- 2023
iliyowasilishwa na kusomwa Ikulu, Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo
alipozungumza kwenye viwanja vya Ikulu, Zanzibar baada ya kuwasilishwa kwa taarifa
ya Mdhibiti na Mkaguzi Kuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar, (CAG).
“Nitatataka kupata
majibu kwa wote waliotajwa kwenye ripoti ya CAG ambao hawakutoa majibu, watoe
ambao watashindwa kufanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa” Alilisitiza Rais
Dk. Mwinyi
Dk. Mwinyi alisema,
ripoti imeonesha mafanikio, changamoto na mapungufu ambayo Ofisi ya CAG iliyabainisha
wakati wa uwasilishwaji wake na kueleza kwamba Serikali itachukua hatua mbali
mbali zikiwemo za kiutawala na kijinai kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa.
“Kwa wale wote
watakaothibitika kufanya ubadhirifu, wizi au uzembe ulioisababishia Serikali
kupata hasara, utaratibu wa kuchukua hatua uko wazi” Alibainisha Dk. Mwinyi.
Alisema, kuna baadhi
ya maeneo yanahitaji kuchukuliwa hatua za kiutawala na baadhi ya kuchukuliwa hatua
za sheria za makosa ya jinai.
Alidha, Rais Dk.
Mwinyi alieleza kwamba ataikabidhi ripori hiyo kwa Mamlaka zinazohusika kwa
hatua zaidi, ikiwemo Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi,
Zanzibar (ZAECA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ili
nao waipitie kwa kina mapungufu yote hasa yaliyoashiria wizi kwaajili ya hatua
zaidi kwa mujibu wa sheria.
Dk. Mwinyi alisema, ripoti
za CAG ni kipimo tosha cha utendaji kwa wale wote waliopewa majukumu na
Serikali kwa kufanikiwa ama kushindwa kuyasimamia katika kuitumikia Serikali.
“Utaratibu huu
tuliouazisha wakuwasilisha ripoti za CAG hadharani utakuwa wadudumu, nafahamu
kuwa haukuzoeleka na unawapa mashaka baadhi ya watu, nataka niwahakikishie kwa
wale wenye mashaka, hili litakua zoezi la kila mwaka, na ni moja wapo ya kigezo
cha uwazi na utawala bora katika uendeshaji wa Serikali yetu” Alitanabahisha
Rais Dk. Mwinyi.
Hata hivyo, aliwataka
watendaji na watumishi wa taasisi na mashirika ya Serikali kuendelea kutoa
ushirikiano wa kutosha kwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali, Zanzibar panapokua na wajibu wa kufanya hiyo. Alisema kutofanya hivyo
ni kosa kisheria na Serikali haitosita kutimiza wajibu wake.
Akizungumzia
mapungufu yaliyojitokeza kwenye ripoti hiyo, Rais Dk. Mwinyi alieleza baadhi ya
mapungufu hayo ni ya kiutaratibu, mengi yalisababishwa na wizi na mengine uzembe
kwa baadhi ya watu.
Hivyo alieleza, kazi
ya CAG kutoa taarifa na mapendekezo kwa Serikali na jukumu la kufanyiakazi
ripoti hiyo ni la Serikali.
Mapema, akiwasilisha
ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Dk. Othman Abass
Ali, aliishauri Serikali kuunganisha pamoja mifumo yote ya fedha ya Serikali,
kwa miamala ya fedha zikiwemo fedha zilizoko Benk kuu ya Tanzania (BOT) kupitia
mifumo ya Wizara ya Fedha kwa lengo la kuiwezesha mifumo hiyo, kufanya
usuluhishi wa upatikanaji wa taarifa za ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa
wakati sahihi.
Sambamba na
kuziunganisha pamoja sekta zote za Serikali zinazofanyakazi zinazofanana katika
mfumo mmoja zikiwemo, Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Zanzibar (ZAA), Kampuni ya Usafirishaji bandarini na nyenginezo ili
kupata idadi kamili ya wageni na abiria wanaoondoka Zanzibar kwa lengo la kuwepo
kigezo sahihi cha ukokotoaji wa ukusanywaji wa mapato yanayotakiwa kupatikana
kutoka kwenye vyanzo hivyo.
Pia aliishauri
Serikali kuongeza udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vitenganishi, ikiwemo kufanya
uteketezaji pamoja na kuvipitia vituo vyote vya afya kwa hospital zote za Wilaya,
Mikoa hadi Rufaa kwa dawa zilizomo hospitalini pia kufanya vipimo vya kimaabara
ili kugundua dawa na vifaa visivyo salama kwa matumizi wa binaadamu kwa kuzichukulia
hatua za haraka na kuziondosha kwa kuziteketeza kwa wakati.
Akizungumzia suala la
kulipa fidia kwa wananchi wanaotoa maeneo yao kwaajili ya kupisha miradi ya
Serikali ya Maendeleo, CAG akiishauri Serikali kuona umuhimu wa kuwalipa kwa
wakati ili kuepusha malalamiko, kucheleweshewa kulipwa kwa wakati kunapunguza
thamani ya fidia kutokana na kupungua kwa thamani ya fedha.
Jumla ya ripoti saba
ikiwemo ya Serikali Kuu (Mawizara na taasisi zote), Mashirika na Taasisi
zinazojitegemea, ripoti ya Idara Maalum na taasisi zake, ripoti ya mifumo yote
ya Tehema ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ripoti ya Mashirika ya Umma, na
ripoti ya Ufanisi ya miradi ya Maendeleo iliyofadhiliwa na fedha za Uviko 19
ziliwasilishwa.
Kifungu cha 112 (5)
kinamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, awasilishe
taarifa yote aliyoikagua na aikabidhi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi kwa hatua nyengine. Mei 11 mwaka huu alivyanya hivyo na
baadae Rais Dk. Mwinyi alimkabidhi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba,
Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman ambae nae aliikadhiri
Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa takwa la kikatiba kwaajili ya kujadiliwa.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment