Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania
TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa, ametoa wito kwa wadau wote wa masuala ya maendeleo ya
jinsia kutumia muongozo wa sera ya jinsia ulioandaliwa kwa ajili ya vyombo vya habari
ikiwemo vyuo vikuu, taasisi za serikali na binafsi ili kuweza kufikia usawa wa
kijinsia.
Dkt. Mzuri ametoa wito huo wakati wa uzinduzi rasmi wa
muongozo wa sera ya jinsia uliofanyika huko katika ofisi za TAMWA ZNZ, Tunguu
Mkoa Kusini Unguja.
Dkt. Mzuri aliongeza kuwa sera ya kijinsia itatambua
kanuni mbalimbali zitakazoundwa na chombo cha habari ambazo kitaipa mamlaka
dawati la jinsia ya kusikiliza na kupokea taarifa mbalimbali za unyanyasaji wa
kingono au viashiria vitakavokuweko sehemu za kazi ili kuweza kuchukua hatua za
kinidhamu.
“Ni lazima tukubali kwamba kazi bila ya unyanyasaji wa
kijinsia inawezekana, hivyo ni lazima kuweko kwa fursa sawa ambazo zitaepuka
ukatili wa kijinsia”.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar ndugu
Suleiman Abdallah amesema ni muhimu kwa vyombo vya habari kufuata na kutumia
muongozo huo wa sera ya jinsia ili kuweza kuweka usawa wa kijinsia katika
maeneo ya kazi lakini pia kuondosha changamoto mbalimbali zinazowakabili
wanawake.
Naye, Mwenyekiti wa Mtandao wa Kijinsia (ZGC) Bi.Asha
Aboud ameipongeza TAMWA-ZNZ kwa kutayarisha na kuzindua muongozo wa sera ya
kijinsia na kuwataka wakuu wa vyuo vikuu hapa nchini kuwa na sera hiyo pamoja
na dawati la kijinsia ili kuweza kuepuka rushwa ya ngono ambayo moja ya athari zake
ni kutoa wasomi ambao hawana sifa.
Sera ya kijinsia imezinduliwa kufuatia utekelezaji wa maradi wa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi (SWIL) ambao unatekelezwa na TAMWA ZNZ, ZAFELA na PEGAO kwa ushirikiano mkubwa wa balozi wa Norway. Mwisho -
No comments:
Post a Comment