Serikali kupitia Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar ipo mbioni kuanzisha Kituo cha Utatuzi wa Migogoro nje ya Mahkama (ADR Center) pamoja na Sheria zinazosimamia uanzishwaji na uendeshaji wa Kituo hicho.
Kukamilika kwa Kituo hicho kutasaidia kutatuliwa kwa
migogoro kwa haraka, na kinatarajiwa kuchochea zaidi ongezeko la Wawekezaji
wanaokuja Zanzibar kwa vile Wawekezaji hao watakuwa na amani na uwekezaji wao
nchini.
Naibu MWANASHERIA Mkuu ZANZIBAR Shaaban Ramadhan Abdalla ameyasema
hayo wakati akifungua Mkutano wa kupokea maoni kuhusu Rasimu ya uanzishwaji wa
Kituo hicho huko katika Ukumbi wa Mikutano wa Afisi hiyo Mazizini uliohudhuriwa
na Wataalam wa Sheria kutoka katika Taasisi za Serikali na binafsi nchini.
Naibu Shaaban amesema Sheria iliopo ya Utatuzi wa Migogoro Sura
Nam. 25 ya mwaka 1928 imepitwa na wakati kwa vile ilianzishwa enzi za ukoloni
na haiendani na kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia ambayo yamefikiwa
nchini.
Amesema kulingana na kasi ya ukuaji wa uchumi, teknolojia na
shughuli mbali mbali za kiuwekezaji Sheria hiyo inahitaji kuimarishwa zaidi ili
kwenda sambamba na kasi ya maendeleo.
“Mambo yatakapokamilika tutaifuta ‘Arbitration decree’ na tutakuja
na ‘Arbitration Act’ pamoja na kanuni ambazo zinasaidia kutatua migogoro kwa wakati
tulionao” alifafanua Naibu Mwanasheria Mkuu.
Amefahamisha kuwa, katika hali ya kawaida migogoro
inapotokea hupelekwa mahkamani lakini kuna baadhi ya migogoro haihitaji kuwa na
taratibu nyingi na za muda mrefu kutatuliwa kwake.
Akitolea mfano Naibu Mwanasheria Mkuu amesema “wote ni
mashahidi namna Zanzibar ilivyojikita katika maswala ya uwekezaji na ujenzi
hasa wa Miundombinu. Kwenye maswala hayo kesi zikipelekwa katika Mahkama za
kawaida zitachukua muda mrefu na hivyo kuathiri uekezaji na uchumi wa nchi.
Sasa tunapokuwa na ADR Center kesi hizo zitapelekwa huko na kupata suluhu kwa
muda mfupi ili kazi ziendelee”.
Kwa upande wake Mrajisi wa Mahkama Zanzibar Valentina Andrew
Katema amesema kuanzishwa kwa Kituo cha Utatuzi wa Migogoro nje ya Mahkama ADR
Center kutasaidia kutatua migogoro kwa haraka na kuipunguzia mzigo Idara ya
Mahkama.
Amebainisha kuwa, utaratibu wa kwenda Mahkamani ni kwenda
kupata hukumu kati ya kushinda au kushindwa jambo ambalo wakati mwingine
haliachi picha nzuri miongoni mwa walioshitakiana mahkamani.
Mrajis huyo ameongeza kuwa, Watu watakapoamua kwenda kutatua
mgogoro wao katika Kituo cha “ADR Center” kuna uwezekano mkubwa wa kubakia
katika mahusiano mema kwa vile hakuna kushindwa wala kushinda bali ni kufikia
makubaliano ya pande zilizokuwa na mgogoro.
Akizungumzia faida za Kituo hicho Bi Valentine amesema
kuwepo kwa ADR Center kutahamasisha shughuli za kiuchumi kwa vile Wawekezaji
watakuja kwa wingi wakijua kwamba kuna namna nzuri ya kusuluhisha Migogoro pale
inapoibuka.
Amesema ADR Center itawapa utulivu Wawekezaji kuona kwamba,
wanayo sehemu nzuri ya kukimbilia pale shughuli za uwekezaji wao zinapoingia
katika migogoro na kupata suluhu kinyume na kupelekana mahkamani.
“Wenzetu wawekezaji wanapokuja kitu cha msingi huzingatia
sana usalama wa uwekezaji wao na hawapendi kupelekwa mahkamani kutokana na
gharama za Mahkama na kuchukuwa muda mrefu sasa ADR Center itawarahisishia kwa
vile kunapotokea shida watafika hapo kwa ajili ya kutatua tatizo nje ya
Mahkama” Amefahamisha Valentina
Aidha amefafanua kuwa, kupitia wingi wa wawekezaji nchini
kutachochea shughuli za kiuchumi na ongezeko la fursa za ajira kwa wananchi.
Kwa upande wake mmoja wa Washauri elekezi Dkt. Fauz Twaib ambaaye
ni Jaji Mstaafu na Rais wa Jumuiya cha Wanasheria Afrika Mashariki amesema lengo
la kazi wanayoifanya ni kuleta Sheria ambayo itaweka masharti ya jinsi gani
Sheria za usuluhishi hasa wa migogoro zinavyotakiwa kufanya kazi Zanzibar kwa
zama za sasa.
Amesema kupitia kazi hiyo wanakusudia kuubadilisha mfumo wa
Sheria hizo za utatuzi wa migogoro ambao kwa sasa sheria yake ina zaidi ya
miaka 100 toka kuanzishwa kwake na kwamba haiendani ten ana hali halisi.
Dkt. Fauz amefahamisha kuwa kazi yao kubwa ni kuandaa sheria
mbali mbali hasa Sheria hiyo ya usuluhishi lakini pia wamependekeza kituo
maalum kwa ajili ya utatuzi wa Migogoro ingawa haitoshughulika na maswala yote
kwa vile migogoro mingine itapelekwa katika Mahkama za kawaida.
Amepongeza maoni yaliyotolewa na na Wadau wa Sheria na kwamba watayachukua na kwenda kuyafanyia kazi ili kuikamilisha Rasimu hiyo ikiwa bora zaidi na kuikabidhi Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar kwa hatua za mbele zaidi.
No comments:
Post a Comment