Habari za Punde

Nitakisimamia chama changu cha CCM kiuchumi - Dk Mwinyi

 

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussain Ali Mwinyi ameahidi kukisimamia chama hicho kiuchumi.

Aliyasema hayo, Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, shehiya ya Bopwe Wete Pemba alipozungumza kwenye Mkutano wa Mabalozi, wajumbe wa Halmashauri za majimbo, Wilaya na Mkoa wa Kaskazini Pemba kichama ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya chama kisiwani humo.

Dk. Mwinyi alisema ili chama kijiendeshe kiuchumi na kuwapatia maslahi watendaji wake wa ngazi zote, lazima kijiekeze kiuchumi kwa kuwa na vitega uchumi vingi kama sehemu ya mapato yake.

Pia alieleza kufurahishwa kwake na rasilimali za chama alizozishuhudia kwenye ziara zake za mikoa yote kichama Unguja na Pemba na kueleza kuzifanyia tathmini kuangalia uwezekano wa  ya kuziendeleza kiuchumi ndani ya chama na baadhi yao kuziwekeza kwa sekta binafsi ili kuziimarisha zaidi na kuongeza mapato ndani ya chama.

Pia, aliahidi kuwa na ofisi mpya za chama zenye hadhi za juu pamoja na vitendeakazi vya ofisini zikiwemo, kompyuta na vifaa vyote vya ofisi, ujenzi wa kumbi kubwa za mikutano zenye uwezo wa kubeba mikutano mikuu ya chama kwa Unguja na Pemba.

Akizingumzia sekta ya maendeleo kisiwani Pemba hususani kuimaisha miundombinu ya barabara, bandari na viwanja vya ndege Pemba alisema amedhamiria kuifungua kiuchumi kwa kuruhusu ndege na meli za kimataifa kuingia Pemba na wawekezaji baada ya kufanywa  marekebisho makubwa ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa kwa bararabara, bandari ya Wete na kiwanja cha ndege.

Alieleza, tayari miradi mingi ya maendeleo imekamilika ndani ya kipindi cha miaka miwili na nusu na kueleza juhudi zaidi zimeelekezwa kuikamilisha miradi iliyobakia ikiwa ni utekelezaji Ilani ya uchaguzi ya CCM, 2020- 2025.

Sambamba na hayo Dk. Mwinyi pia alikiagiza chama kutoa mafunzo kwa vongozi wepya ilikuwajengea uwezo katika utekelezaji wa kazi za chama hicho pamoja kukitaka kutayarisha mpango maalumu wa kuwatambulisha majukumu viongozi wapya, aidha, aliwaagiza kufanya vikao vya kikatiba ili kushughulikia mapema changamoto zinazokikabili chama kwaajili  ya kuzitatua kwa wakati.

Naye, Naibu Katibu Mkuu CCM, Zanzibar, Mohamed Said Muhamed (Dimwa) alimueleza Makamu Mwenyekiti Dk. Mwinyi kwamba maagizo yote aliyayatoa ndani ya chama tayari yametekelezwa ikiwemo kuwapatia vitambulisho mabalozi wote wa CCM na watendaji wa ngazi zote kwaajili ya zoezi la kuanza kuwapatia maslahi yao.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba, Salama Mbaruok Khatib ndani ya kipindi cha miaka miwili  na nusu cha utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM, 2020-2025 Kaskazini Pemba imepiga hatua kubwa kimaendeleo kwenye sekta zote zikiwemo maji elimu, afya miundombinu na michezo aliongeza ujenzi wa barabara mpya  za nje na ndani unaendelea kwa kasi hubwana tayari serikali imewalipa fidia wananchi wa maeneo yote waliopitiwa na barabara.

Mapema akizungumza kwenye Mkutano huo Mwenyekiti wa CCM, Mkoa Kaskazini Pemba,  Mberwa Hamad Mberwa, alieleza  hali ya amani, umoja na mshikamo kwa mkoa huo bila kujali tofauti ya itikadi za vyama.

Aidha, alieleza ushirikiano mkubwa wa viongozi wa chama na serikali kwa mkoa wa kaskazini huo katika kutekeleza maendeleo na kueleza walivyokabiliana na kasoro ndogo ndani ya chama chao.

Akiwa kwenye mwendelezo wa ziara yake kichama Mkoa wa Kaskazini Pemba, Makamu Mwenyekiti Dk. Mwinyi pia alitembelea mali na vitega uchumi vya chama ndani ya mkoa huo, ukiwemo ujenzi wa jengo la ghorofa nne Micheweni litakalogharimu shilingi 1.187 bilioni litalohusisha maduka, ofisi za chama na nyumba za biashara kama kitega uchumi cha chama

Pia Dk. Mwinyi alitembelea mali za chama za Jumuiya ya Wazazi shehia ya Machengwe Mkoa wa Kaskazini Pemba viwemo viwanja.

Ziara ya Kaskazini Pemba imekamilisha ziara ya Makamu Mwenyekiiti Dk.Mwinyi ya  kutembelea rasilimali za chama hicho zikiwemo mali majengo na vitegauchumi vyake kwa mikoa yote mitano ya Unguja na Pemba kichama.

IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.