Habari za Punde

Mhe Hemed aendelea na ziara ya kukagua uhai wa chama majimbo ya Chaani, Mkwajuni na Tumbatu Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kuachana na watu ambao wanawabeza viongozi kwa kuwakashifu na kuwasema vibaya juu ya jitihada zao wanazozichukua za kuwaletea maendeleo wananchi.

 

Ameyaeleza hayo wakati akizungumza na viongozi, wanachama wa CCM na wananchi wa Majimbo ya Chaani, Mkwajuni na Tumbatu Wilaya ya Kaskazini A ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Unguja. 

 

Amesema wapo baadhi ya Viongozi wa Vyama vya upinzani ambao wana malengo ya kukichafua chama na viongozi wake hivyo ni vyema kwa wana CCM kuwapuuza na kuendelea kuwa wamoja na kukiimarisha Chama kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.

 

Amesema majimbo yaliyomo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja yatabaki kuwa ni ngome ya CCM na hatotokea mpinzani yoyote kuongoza katika Majimbo hayo hivyo umoja, upendo na mshikamano ndivyo vitakavyokiletea Chama Cha Mapinduzi ushindi wa kishindo katika Uchaguzi wa Dola ifikapo mwaka 2025.

 

Aidha amefahamisha kuwa, Viongozi wa Majimbo wanafanya kazi kubwa za kimaendeleo na kuitekeleza vyema Ilani ya CCM, hivyo ni busara kuachana na makundi, Majungu na Mifarakano ndani ya chama ili kutowapa mwanya wapinzani wa kujiegemeza katika ngome za CCM.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kaskazini "A" Ndugu Ali Makame Khamis Ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Awamu zote kwa kusimamia Misingi ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Muungano wa Tanzania.

 

Awali Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alikabidhi kwa Mwenyekiti wa Jimbo la Chaani vifaa vya ujenzi ikiwemo matofali 200, saruji mifuko 100, gari 10 za mawe, gari 2 za kifusi na mchanga gari moja vilivyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Chaani Mhe. Nadir Abdullatif kwa ajili ya ujenzi wa Tawi la CCM Pwani Mchangani B na Ujenzi wa Kituo cha Afya Kandwi.

 

Akikabidhi vifaa hivyo Mhe. Hemed amewataka viongozi kuvitumia vifaa hivyo kama ilivyokusudiwa na hatafumbiwa macho yoyote Yule atakaevitumia vifaa hivyo kinyume na ilivyokusudiwa.

 

Mhe.Hemed amefurahishwa na hatua za kimaendelea zilizotekelezwa na Viongozi wa Majimbo ya Mkoa wa kaskazini Unguja kwa kuitekeleza kwa vitendo ilani ya CCM. 

 

Nao viongozi wa Majimbo ya Chaani, Mkwajuni na Tumbatu wamemuahidi Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kuwa CCM haihitaji kutumia nguvu kubwa katika kuomba kura mwaka 2025 kutokana na misingi imara ya kuwatumikia wananchi.

 

Wamesema Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Unguja kimejipanga kimkakati kuhakikisha wananchi wanakipigia kura Chama Cha Mapinduzi ili kuendelea kukiweka madarakani Chama hicho ifikapo mwaka 2025 .

 

Katika Ziara hiyo Mhe. Hemed amepokea Taarifa za Utekelezaji wa Majimbo hayo na kukagua ujenzi wa Tawi la CCM Kandwi, amefungua Maskani ya CCM Matemwe Pani na ameshiriki ujenzi wa Tawi la CCM Kipange Muembe Duka.

 

 

…………………………….

LULUWA SALUM

AFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR

19/08/2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.