Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Wingwi na Jimbo la Micheweni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali imo mbioni kukamilisha mpango maalum wa elimu ambao utawanufaisha Watanzania kupata elimu katika ngazi zote kuanzia Maandalizi, Msingi, Sekondari hadi Vyuo Vikuu.
Amesema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kutekeleza Ilani ya CCM Kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kuwaletea wananchi maendeleo hasa katika sekta ya elimu, Afya, Miundombinu na barabara.
Amefahamisha kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha Vijana waweze kujiajiri badala ya kusubiri ajira kutoka Serikalini na kuwataka wawe makini na wapinga maendeleo ambao hawaitakii Nchi maendeleo.
Ameeleza kuwa maendeleo yoyote yanahitaji uwepo wa mazingira thabiti ikiwemo miundombinu mbali mbali kama vile maji na barabara ambapo Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi itahakikisha inazijenga barabara zote kwa kiwango cha Lami.
Amesema vijana ndio tegemeo la Chama Cha Mapinduzi hivyo waendelee kukijenga Chama makini ambacho ndicho kitakachoendelea kuwakomboa na kuwatimizia ndoto zao za kimaisha yao.
Mhe. Hemed amefahamisha kuwa umoja, ushirikiano na upendo ndivyo vitakavyokivusha Chama Cha Mapinduzi hivyo Viongozi na wana CCM wanapaswa na kuendelea kufanya kazi ya kukiimaricha Chama hicho.
Amefafanua kuwa Viongozi na wanachama wa CCM wanapaswa kubadilika kuelekea katika siasa za kisasa katika kuongoza Dola na hii ndio itakifanya Chama Cha Mapinduzi kushinda katika ngazi zote za uongozi katika uchaguzi Mkuu ujao 2025.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mhe. Salama Mbarouk Khatibu amesema Mkoa huo umejipanga kuanzisha Mradi wa kujenga mabwawa kumi na nane (18) ya kufuga majongoo na kamba pamoja na mradi wa ufugaji kuku ambao vijana elfu moja na mia moja (1,100) wataweza kujiajiri kupitia miradi hiyo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
No comments:
Post a Comment