Habari za Punde

SMZ Imedhamiria Kuwaletea Maendeleo Wananchi Wote wa Zanzibar -Mhe.Hemed

Mjumbe wa Kamti Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuwaletea maendeleo wananchi wote wa Zanzibar kupitia sekta mbalimbali bila ya kujali tofauti ya aina yoyote.

Mhe. Hemed ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi, wanachama wa CCM na wananchi wa Jimbo la Chake chake alipokuwa  akihitimisha ziara yake ya Majimbo Hamsini ya Uchaguzi ya Zanzibar.


Amesema dhamira ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ni kuijenga Zanzibar katika nyanja zote kiuchumi, kisiasa na jamii ili wananchi wawe na mazingira mazuri yaliyo bora.


Amefahamisha kuwa Serikali itahakikisha Kiwanja cha michezo cha Tibirinzi kinajengwa cha kisasa chenye hadhi ya Kimataifa ili kuibua vipaji na kukuza michezo nchini.


Mhe. Hemed ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali imeanza ujenzi wa Viwanja vya michezo vya kisasa kila Wilaya ambacho ujenzi wa Kiwanja cha Tibirinzi kitatoa fursa kwa vijana wa maeneo ya Chake chake na maeneo jirani kuweza kukitumia.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema malengo ya Rais Dkt. Mwinyi ni kuufanya Mji wa Chake chake kuwa ni sura ya Kisiwa cha Pemba ambapo kukamilika kwa Bustani ya kupumzikia eneo la Mwanamashungu, ujenzi wa Barabara kutoka Chake hadi Wete pamoja na miundombinu ya Taa za Barabarani kutasaidia kuweka haiba nzuri ya mji huo.


Amesema Serikali ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi zinasogeza huduma za kijamii maeneo yote ili wananchi wote wanufaike na uwepo wa Serikali zao.


Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ameupongeza Uongozi wa Jimbo la Chake chake kwa mashirikiano mazuri waliyonayo baina ya Serikali na Chama na kuwataka wanachama kuungana na viongozi wao katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.


Sambamba na hayo amezishukuru Kamati zote za Siasa kuanzia Tawi hadi Mikoa kwa maandalizi mazuri ya ziara katika majimbo yote Hamsini hatua ambayo inaonesha utayari wa viongozi hao katika kukiimarisha Chama.


Akizungumza kwa niaba ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Bi Zawadi Suleiman amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuendelea kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa kujenga miradi mingi ya maendeleo.


Wamewaomba wananchi kuthamini juhudi zinazofanywa na viongozi wetu kwa kulinda miradi hiyo ili idumu kwa muda mrefu na iweze kufaa kizazi cha sasa na kizazi vijavyo.


Nae Muwakilishi wa Jimbo la Chake chake Mhe. Hassan Shaibu Kaduwara na Waziri wa Maji Nishati na Madini ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi wa Zanzibar anapata huduma ya Maji safi na Salama kwa muda wote.


Ameeleza kuwa ndani ya miaka Miwili ya Awamu ya Nane Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) imeweza kuzalisha Maji Lita Milioni Mia moja Arobaini na Tisa (149,000,000) ikilinganishwa na Lita Arobaini na Nane (48) iliyokuwa ikizalishwa awali hatua ambayo itaweza kusaidia kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa Nchini.


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amekamilisha ziara yake ya kuimarisha Chama katika Majimbo yote Hamsini ya Uchaguzi Unguja na Pemba aliyoianza Tarehe 29 Julai mwaka huu Mkoa wa Magharibi Kichama Jimbo la Kiembesamaki.


Katika ziara yake hiyo Mhe. Hemed amekagua na kushiriki ujenzi katika Matawi, Maskani na maeneo ya vitega uchumi ya CCM, amepokea taarifa za utendaji kila Jimbo, amepokea wanachama wapya na kutoka upinzani, pamoja na kuzungumza na Viongozi, wanachama na wananchi kwa majimbo hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.