Habari za Punde

Karibuni kuwekeza Tanzania - Mhe Othman


 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa ni pahala bora, salama, na miongoni mwa sehemu zenye mazingira rafiki ya uwekezaji ulimwenguni.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo, wakati akiufunga rasmi Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Nishati, huko katika Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam Tanzania.

Amesema Dunia imeishuhudia Tanzania ya sasa ikiwa ni kigezo cha amani kwa muda wa miongo kadhaa kutokana na utulivu wake wa kisiasa sambamba na mazingira yake bora ya asili, ambavyo ni vichocheo muhimu kwaajili ya uwekezaji wa sekta mbali mbali za kiuchumi.

Akiwakaribisha Wawekezaji mbali mbali wakiwemo wa Sekta za Nishati, Mafuta na Gesi, Mheshimiwa Othman amekaririwa akisema, “kutokana na uhalisia kwamba sisi tumekuwa ni kigezo cha amani kwa miongo kadhaa; kwa udhati tumekuwa miongoni mwa Nchi zenye utulivu wa kisiasa ulimwenguni; tunayo furaha kubwa kukwambieni kwamba kila mmoja wenu, na kwa nia njema ya uwekezaji iwe katika Nishati au vinginevyo katika sekta za maendeleo, karibuni njooni muwekeze katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bara na Zanzibar”.

 

Akieleza juu ya Sekta ya Nishati Nchini, Mheshimiwa Othman amesema, kama ilivyo kwa Tanzania Bara, sambamba na Mikakati Maalum ya Uwekezaji, mathalan Sera za Uchumi wa Buluu, Zanzibar nayo inahitaji Wawekezaji Makini na Washirika wa Kimataifa watakaowezesha Mabadiliko ya Kweli katika Sekta za Nishati, Gesi Asilia na Mafuta kupitia  Mapinduzi muhimu ya Teknolojia na Ukuzaji wa makusudi wa fursa za ajira unaokwenda sambamba na Soko la Dunia.

 

Aidha, Mheshimiwa Othman pamoja na kubainisha fursa hizo, amewakaribisha Wawekezaji na Wajumbe wa Mkutano huo, kutenga muda angalau wa kujionea Vivutio mbali mbali vya Utalii ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vikiwemo vya Mlima Kilimanjaro, Mbuga za Serengeti na Ngorongoro, na pia Fukwe na Mandhari Nzuri ya kuvutia na ya kihistoria katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

 

Awali kabisa, Mheshimiwa Othman alipata nafasi ya Kukagua Mabanda ya Maonyesho hapo,  yanayohusu Kazi za Ubunifu wa Nishati, ambayo yamekwenda sambamba na Mkutano huo.

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Dotto Mashaka Biteko (MP), amesema Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Nishati ni fursa muhimu ya kutanua wigo katika nyanja mbali mbali za uwekezaji, kwaajili ya kuinua uchumi wa Nchi husika.

 

Mheshimiwa Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati, katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amefahamisha kuwa kwa vile Mkutano huo umewakusanya Wadau wote Muhimu wa Sekta za Uwekezaji, katika Ngazi za Taifa, Kanda, Bara la Afrika, na kwengineko Duniani, matumaini yaliyopo ni pamoja na Kwamba Maazimio na Mapendekezo yatalenga kuibua fursa za Uwekezaji wa Miradi Mikubwa ya Nishati, kwaajili ya Maendeleo ya Mataifa husika.

 

Naye, Mkurugenzi wa 'Ocean Business Partners' ambao ni Wenyeji wa Mkutano huo wa Kimataifa wa Siku Mbili, Bw. Abdulsamad Abdulrahim, ameeleza matumaini makubwa kwa Nchi wahusika zilizojumuika hapo, kupitia fursa nyingi ziliopo, zikiwemo za ajira na Uwekezaji wa Miradi Mikubwa, baada ya maazimio na mipango ya baadae, katika kukuza na kuimarisha Sekta ya Nishati kwa maslahi pia ya Uchumi wa Taifa na Mataifa mengine husika.

 

Amepongeza juhudi zinazochukuliwa na Marais wote Wawili, Dokta Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Dokta Hussein Ali Mwinyi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa juhudi zao za Makusudi, kwa kuhakikisha kwamba Taifa linafungua Milango ya Uwekezaji wa Miradi Mikubwa, ikiwemo ya Sekta za Nishati, Gesi Asilia na Umeme.

 

Pamoja na Mambo mengine, Wajumbe wa Mkutano huo kutoka takriban Nchi 93 Duniani, wamejadili kwa kina, pamoja na kuweka mapendekezo, juu ya Usambazaji wa Gesi Asilia (LNG); Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP); Ubunifu wa Nishati Endelevu; Mbinu Mbadala katika Uzalishaji wa Nishati; na Namna bora ya Ufadhili wa Miradi Mikubwa ikiwemo ya Nishati, ndani na nje ya Bara la Afrika.

 

Wanadiplomasia, Wasomi na Wataalamu, Wawakilishi kutoka Mashirika ya Kimataifa, wakiwemo pia  kutoka Jamhuri za Indonesia, Malawi na Uganda, Washirika wa Maendeleo na Wafadhili, Mawaziri na Makatibu Wakuu kutoka Wizara mbali mbali, Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Watendaji na Viongozi mbali mbali wa Serikali zote Mbili, za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, pamoja na Asasi za Kiraia, wamehudhuria katika Mkutano huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.