RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezitaka taasisi
zote zinazohusiana na usimamizi wa sekta ya Utalii nchini, kuhakikisha
wajasiriamali wa ndani wanapewa kipaumbale kunufaika na fursa zinazopatikana
kwenye sekta ya utalii hususan masoko ya bidhaa wanazozalisha.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo alipofungua tamasha la Fahari ya Zanzibar
sambamba na maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa taasisi ya Wakala
wa Uwezeshaji wa nchi kiuchumi Zanzibar (ZEEA) kwenye hoteli ya Golden Tulip,
Uwanja wa ndege Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alisema hali hiyo itapunguza kwa kiasi kikubwa uingizaji wa bidhaa kutoka
nje ya nchi zinazoweza kuzalishwa Zanzibar na kuimarisha soko la ndani kwa
wajasiria mali wake.
“Nazika taasisi zote
zinazohusiana na usimamizi wa sekta ya utalii nchini, kuhakikisha wajasiriamali
wa ndani wawe wanufaika wa kwanza kwa fursa zinazopatikana kwenye sekta ya
utalii, hali hiyo itapunguza kwa kiasi kikubwa uingizaji wa bidhaa tunazoweza
kuzizalisha, kutoka nje ya nchi na kuimarisha soko la ndani kwa wajasiria mali
wetu” Aliagiza Rais Dk. Mwinyi.
Rais Dk. Mwinyi alisema juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi ni
kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya Zanzibar kwa bidhaa wanazozizalisha,
aliongeza uchumi wa Zanzibar una fursa nyingi za masoko kwa bidhaa za
wajasiriamali wake kutokana na kuwepo kwa hoteli nyingi za utalii.
Dk. Mwinyi aliwataka
wajasiriamali na wafanyabiashara wa ndani kushirikiana na wadau wengine
kuzalisha bidhaa zenye ubora kulingana na mahitaji na kunufaika na soko la
utalilii liliopo.
Aliongeza, suala la kuwawezesha wananchi kiuchumi ni mtambuka kwa vile
linahusisha wadau wengi na sekta mbalimbali zikiwemo Uchumi wa Buluu, Kilimo,
Utalii, Biashara, taasisi za fedha, sekta binafsi na asasi zisizo za serikali
za kitaifa na kimataifa.
Pia Rais Dk. Mwinyi alieleza taasisi zote hizo zina wajibu na dhima ya
kutengeneza fursa za ajira kwa maendeleo ya Zanzibar yanayokwenda sambamba na
sera ya taifa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ya mwaka 2022.
Alisema, adhma ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha ongezeko la ajira kwa vijana
na wanawake linaongezeka kwa kuendelea kutoa fursa nyingi na kuwawezesha
kiuchumi kutokana na fursa za mikopo zilizopo.
“Serikali
imejidhatiti kutimiza malengo ya ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 /2025 ya
kuzalisha fursa za ajira laki tatu kwa kipindi cha miaka mitano, ni dhahiri
kasi iliopo idadi hii haiwezi kusalishwa na ajira kutoka serikalini pekee bila
shaka fursa nyingi za ajira zitatokana na kuwawesha wananchi kujiajiri ambapo
wajibu wa Serikali ni kuandaa mazingira wezeshi kwa wananchi wake ili
kujikwamua” alieleza Rais Dk. Mwinyi.
Alisema, Serikali
inaendelea na hatua ya kuimarisha na kuinua maeneo ya biashara ikiwemo ujenzi
wa masoko na maeneo muhumu ya kufanyia biashara kwenye maeneo ya vituo vya
mabasi, lengo ni kuwapatia wafanyabiashara hao wateja wengi wa bidhaa zao
kwenye maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.
Alisema tamasha hilo
ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha na kuwaweka pamoja wadau wote pamoja na
wajasiriamali mbalimbali kwa kubadilishana uzoefu kwenye tasnia hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga alieleza lengo na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuendelea kutoa mikopo isiyo na riba kwa
wananchi wake na kuwawezesha wajiajiri kupitia mikopo inayowapatia na kuyafikia
malengo yao kiuchumi.
Alisema Wizara
ilijipangia kuwakopesha wajasiriamali 12,000 kwa mwaka na sasa imefikia idadi
ya 19,000 nakuongeza kuwa kiasi cha bilioni 20.2 zimekopeswa kwa wananchi
nakueleza mahitaji yameongezeka zaidi kutokana na maombi ya wananchi wengi
yamefikia bilioni 80.
Akizungumza kwenye
hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji wananchi Kiuchumi, Juma
Burhan Muhamed alisema taasisi hiyo imeingia makubalianao na taasisi mbalimbali
wezeshi kwa wananchi zikiwemo, Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF),
Zanzibar Maisha Bora Foundation, Tan Trade na taasisi nyengine ili kuwainua
wajasaliriamali wa ndani wakiwemo vijana, wanawake na wakulima wa mwani kwa
kuendelea kuwatafutia soko la bidhaa wanazozizalisha.
Pia alieleza taasisi
hiyo inaongeza uelewa kwa jamii kuthamini na kutumia bidhaa zinazozalishwa
ndani ambapo wajasiriamali 19,373 walikopeshwa kiasi cha shilingi bilioni 20.2
kwa Unguja na Pemba.
Wakala wa uwezeshaji
wananchi kiuchumi Zanzibar ni taasisi iliyoundwa mwezi Machi mwaka 2022 ikipewa
jukumu la kutekeleza na kuratibu, shughuli zote za uwezeshaji wananchi
kiuchumi.
IDARA YA MAWASILIANO IKULU,
ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment