Na Rahma Khamis Maelezo 16/9/2023
Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe, Tabia Maulid Mwita ameitaka Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kuweka sheria ndogondogo zitakazowabana wanaochafua fukwe za bahari ili kutunza mazingira nchini.
Wito huo ameutoa wakati akizundua na kushiriki zoezi la usafi katika Fukwe za Maruhubi Wilaya ya Mjini ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Usafi Dunani.
Amesema usafi wa mazingira hasa katika fukwe za bahari ni njia moja wapo ya kuvutia Watalii kufika Zanzibar hivyo kuwepo kwa sheria hizo zitasaidia kuongeza pato la Tafa linalotokana na wageni hao.
Aidha amewataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kusimamia na kuhakikisha suala la usafi linaimarika katika maeneo yote ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na uchafu.
Waziri Tabia amefahamisha kuwa taka ni ajira kwa wananchi hivyo ni wajibu wa Taasisi husika kuhakikisha taka hizo zinatunzwa na kuhifadhiwa katika sehemu salama ili kuepusha uchafuzi wa mazingra.
Aidha amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kuhakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu na kutoa elimu kwa watumiaji wa fukwe juu ya umuhimu wa kutunza fukwe ili kuepusha madharayanayoweza kujitokeza.
Hata hivyo Waziri amewashukuru Wadau waliochangia vifaa vya usafi jambo ambalo litasaidia kuimarisha huduma za usafi na kuwataka wananchi kushirikiana katika kuhimizana suala la usafi kwa vile Zanzibar ni kitovu cha utalii.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Fatma Mbarouk amesema wageni wengi bado hawaridhishwi na hali ya usafi wa Mji hasa katika fukwe hivyo amewataka wadau wa usafi kuongeza jitihada kuhakikisha hali hiyo inaondoka.
Nao wananchi wa maeneo hayo wamesema usafi ni swala la msingi katika jamii hivyo kila mmoja ana haki ya kutekeleza wajibu wake kwa kuimarisha katika eneo lililomzunguka.
Aidha wamefahamisha kuwa sehemu ambayo haina usafi maradhi hayakosekani hivyo wamewaomba wananchi wenzao kushiriki katika suala la usafi ili kujikinga na madhara yanayoweza kuepukika.
No comments:
Post a Comment