RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwasalimia Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, akiwa katika ziara yake katika Mkoa huo kutembelea Miradi ya Maendeleo leo 23-10-2023, baada ya kuifungua Hospitali ya Wilaya Kivunge.
SERIKALI ya
Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kuweka mfumo wa Rufaa kwa hospitali zote za
wilaya nchini.
Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyasema
hayo kwenye ziara ya kuutembelea mkoa wa Kaskazini Unguja alipozindua hospitali
ya Wilaya, Kivunge.
Alisema, Serikali
imeweka utaratibu huo kwa lengo la kuimarisha huduma bora za Afya ziwe za
uhakika zikiwemo Maabara, X-ray, ultrasound mashine za kisasa na dawa na
nyengine kwa maradhi yote ya kawaida ikiwemo uzazi, huduma za uchunguzi na
mengine ili kupunguza msongamano kwenye hospitali kuu ya Mnazi Moja.
Aidha, aliwataka
wananchi wote kurejesha imani zao kwa hospitali za Serikali kwani sasa zinatoa
huduma bora na zina dirisha maalum za mfuko wa bima ya afya na kuwasisitiza
watoa huduma kwenye hospitali hizo kuharakisha huduma zao sio kuweka
misongamano ya wagonjwa.
Pia, Rais Dk. Mwinyi
aliwatoa hofu watumishi wa Serikali na ajira zao na kuwaeleza licha ya Serikali
kushirikisha sekta binafsi kwenye hospitali hizo ajira zao zitaendelea kuwa salama.
Vilevile, Dk.
Mwinyi alihimiza umuhimu wa kuweka kambi maalumu na wataamu wa maradhi
mbalimbali ikiwemo macho, moyo, meno na mifupa.
Naye, Waziri wa
Afya, Nassor Ahmed Mazrui alisifu juhudi za Rais Dk. Mwinyi kuimarisha miundombinu
ya sekta ya Afya kwa ujenzi wa hospitali 10 za Wilaya Unguja na Pemba pamoja na
hospitali moja ya Mkoa.
Akiwa ziarani
Mkoa wa Kaskazini Unguja, Rais Dk. Mwinyi aliweka jiwe la msingi kwenye ujenzi
wa Skuli ya msingi ya ghorofa mbili Donge, itakayokuwa na madarasa 29, ofisi za
walimu, mwalimu mkuu, vyumba vya maktaba, maabara, vyumba vya TEHAMA (ICT), vyoo,
stoon na chumba cha kusalia.
Pia, Rais Dk.
Mwinyi alisifu juhudi za maendeleo zilizofikiwa na sekta ya elimu, Zanzibar kupita
malengo ya ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025 ikiwemo kukamilika kwa skuli
za kisasa za ghorofa na madarasa yatakayochukua wanafunzi 45 kwa mkondo mmoja
tuu.
Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa, alipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kwa kuimarisha miundombinu ya kisasa kwenye sekta ya elimu ndani ya
kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Dk. Mwinyi kwa kuwa na miradi ya
kimkakati ya skuli za kisasa.
Kwa upande wake
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mahmoud alieleza mafaniko ya mkoa huo ikiwemo
kuimarika sekta za miundombinu ya barabara, bandari pamoja na huduma za jamiii,
maji safi, vituo vya afya, kukamilika kwa soko la kisasa Donge Mtambile
litakalotosheleza mahitaji wa wananchi wa eneo hilo na maeneo jirani.
Alisema, Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa michango mkubwa kutekeza miradi mikubwa ya
maendeleo ya mkoani humo.
Ziara ya Rais
Dk. Mwinyi Mkoa wa Kaskazini Unguja ni mwendelezo wa ziara zake za kukagua miradi
ya maendeleo ikiwa ni kuanza shamrashamra na sherehe za mafaniko ya uongozi
wake unaotimiza miaka mitatu.
IDARA YA
MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment