Habari za Punde

Dk.Mwinyi Amewaahidi Wanzanzibari Kuwapunguzia Umasikini Kabla ya Mwaka 2025 kwa Kuwaongezea Miradi Mikubwa ya Maendeleo.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewaahidi Wanzanzibari kuwapunguzia  umasikini kabla ya mwaka 2025 kwa kuwaongezea miradi mikubwa ya maendeleo.

Amesema, amekusudia kuikamilisha kwa vitendo Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025 kwa miaka miwili iliyobakia ya uongozi wake na kuikamilisha miradi mkikubwa ya kimkakati ya Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, barabara za kutulia na kurukia ndege pamoja na jengo kubwa la abiria katika uwanja wa ndege wa Pemba vinavyotarajiwa kugharimu zaidi ya dola za Marekeni milioni 400.

Dk. Mwinyi ambae ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, CCM- Zanzibar aliyasema hayo, viwanja vya Maisara Suleiman Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, alipozungumza na Wazanzibari kwenye maadhimisho ya miaka mitatu ya uongozi wake, tokea alipoingia madarakani kuiongoza awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mwezi Novemba mwaka 2020.

Pia, Rais Dk. Mwinyi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa mchango mkubwa alioutoa kwa maendeleo ya Zanzibar na kuongeza kuwa hatua ya maendeleo iliyofikiwa  ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba kuna mkono wa Rais Dk. Samia.

Akizungumzia suala la amani, umoja na mshikamano, Rais Dk. Mwinyi alisema maendeleo makubwa yaliyofikiwa Zanzibar ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, yametona na juhudi kubwa ya wananchi wa Zanzibar, kuendelea kuidumisha amani iliopo, umoja na mshikamano wao, umetoa fusra nzuri ya kutendeka mafanikio yote hayo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliahidi kuongeza tena kasi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka miwili iliyobakia. Pia aliwapongeza Umoja wa Wanawake Tanzania, (UWT) kwa kazi kubwa wanayoifanya nchi nzima, kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM na miradi ya Maendeleo Tanzania bara na visiwani.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyeketi wa UWT Taifa, Merry Chattanda alipongeza juhudi kubwa ya mafanikio iliyofikiwa na awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye sekta zote za maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabra, Skuli, hospitali 10 za wilaya na moja ya mkoa iliyokamilishwa kwa miundombinu na vifaa vya kisasa, ongezeko la ajira kwa vijana kupitia sekta za ujenzi wa miundombinu, utalii, ujasiriamali, biashara na kilimo cha umwagiliji wa mpunga, hali aliyoielezea matarajio ya Zanzibar kujiwekea akiba ya chakula.

Pia, Chattanda alimpongeza Rais. Dk. Mwinyi kwa kufanikiwa kuwakomboa wanawake wa Zanzibar dhidi ya changamoto cha maji safi na salama kwa kuwajengea visima vikubwa vya maji, Unguja na Pemba pamoja na kuwasambazia mabomba, kuwawekea usafiri wa haraka baharini kisiwani Pemba.

Aidha, Chattanda alisifu mchango mkubwa unaotolewa na Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora             Foundation kupitia Mwenyekiti wake wa Bodi, Mama Mariam Mwinyi, Mke wa Rais wa Zanzibar kwa kuwezesha kinamama wengi wakulima wa mwani na kuwajengea kiwanda kikubwa cha kusarifu mwani, eneo la Chamanangwe, Pemba.

Mapema, akiwasilisha salamu za Chama cha Mapinduzi viwanjani hapo, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Abdul Rahman Kinana aliwasihi Wazanzibari kuendelea kuidumisha amani na mshikano uliopo baina yao na kuendelea kushirikiana na viongozi wao wa Serikali kuijenga Zanzibar.

Sherehe za maadhimisho ya miaka mitatu ya mafanikio ya awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilliandaliwa na kufanikishwa na Jumuiya ya CCM ya Umoja wa Wanawake, Tanzania (UWT)

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.