Na Fauzia Mussa , Maelezo
Mkoa wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe Idrissa Kitwana Mustafa amewataka Watendaji wa ngazi za Wadi na Shehia kuyatumia matokeo ya Sensa ya watu na makaazi katika kuleta maendeleo kwenye maeneo yao.
Akizungumza na Masheha na Madiwani wakati akifungua kikao cha usambazaji na matumizi ya matokeo ya viashiria vya Sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022 huko Polisi Ziwani Mkuu huyo alisema endapo matokeo hayo yatatumika vizuri jamii itaweza kupanga mipango ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
Aidha alisema Takwimu ya idadi ya watu itasaidia katika kuweka rasilimali ambazo zinatumika katika kukuza Uchumi wa Taifa na kupatikana kwa huduma za jamii kwa urahisi hivyo aliwataka Viongozi hao kutumia matokeo hayo katika ugawaji wa rasilimali kwa lengo la kuleta maendeleo Nchini.
Sambamba na hayo alitoa wito kwa Masheha na Madiwani kuwa Mstari wa mbele katika kufikisha taarifa hizo kwa jamii ili kusaidia Serikali katika kutoa huduma sahihi kwa wananchi.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar Salum Kassim Ali alisema Matokeo ya Sensa ni Muhimu kwani yanasaidia kupanga, kusimamia pamoja na kubadilisha maisha ya Wananchi.
Alisema taarifa zinazotolewa na Wananchi ndizo zinazoiwezesha Serikali kubadilisha hali za Wananchi kwa kuwaletea Maendelo,hivyo kuna kila sababu ya Wananchi kupatiwa uwelewa wa umuhimu wa kutoa taarifa sahihi ili kueka mipango madhubuti katika upatikanaji wa huduma ikiwemo huduma za Afya.
Kwa upande wake kamisaa wa Sensa anaefanyia kazi zake Zanzibar Balozi Hamza Haji Hamza amesema kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya watu na makaazi ya mawaka 2022 imeonesha kuwa Mkoa wa Mjini Magharibi una idadi kubwa ya wakaazi ukilinganisha na mikoa mingine ya Zanzibar.
Hata hivyo aliwapongeza Masheha kwa kufanikisha kazi ya sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022 kuanzia matayarisho hadi kupatikana kwa matokeo mazuri.
Katika kikao hicho mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo matokeo muhimu ya baadhi ya Viashiria vya kiuchumi ,Kijamii na mazingira vitokananvyo na sensa ya watu na makaazi
No comments:
Post a Comment