Habari za Punde

Serikali Yaahidi Kuwekeza Zaidi Katika Miradi ya Maendeleo ya Uchumi wa Buluu

Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Dkt. Aboud Suleimani Jumbe akizungumza na Ujumbe wa Shirika la Maendeleo ya Kilimo Duniani (IFAD) pamoja na timu ya Uratibu wa Programu ya AFDP Ofisini kwake baada ya Kumaliza utembeleaji wa Miradi ya Maendeleo inayofadhiliwa na shirika hilo kwa Visiwa vya Pemba na Unguja.


Na Mwandishi wetu Zanzibar.

Imeelezwa kwamba ufugaji wa Nyuki unaweza kuunganishwa na buluu kaboni katika hifadhi ya mikoko na katika ufugaji wa viumbe maji katika maeneo mbalimbali katika kuelekea maendeleo endelevu.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Dkt. Aboud Suleimani Jumbe wakati akizungumza na Ujumbe wa Shirika la Maendeleo ya Kilimo Duniani (IFAD) pamoja na timu ya Uratibu wa Programu ya AFDP Ofisini kwake Mjini Unguja.

“Kufungamanisha maeneo jumuishi yenye miradi tofauti ya uchumi Utasaidia kupata mwamko mkubwa wakujikita katika shughuli za kiuchumi,” amebainisha.

Ziara hii ya Ujumbe wa Shirika la Maendeleo ya Kilimo Duniani (IFAD) pamoja na timu ya Uratibu wa Programu ya AFDP imeonesha namna ambavyo serikali inaweza kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha dhamira ya Miradi ya Maendeleo inafanikiwa.

Aidha upo umuhimu wa kuendelea kuwawezesha wajasiriamali wetu na wakulima wetu wa mwani, wavuvi wadogo wadogo lakini pia haja ya kukabiliana na taka ngumu na maji taka katika bahari.

“Programu ya AFDP ni sehemu kubwa ya ajenda yetu ya maendeleo ya Uchumi buluu na ni ajenda ambayo viongozi wetu wa taifa wamekuwa wakifuatilia kwa karibu sana; ili kuhakikisha malengo yake yanafikiwa kwa wakati” amesema.

Awali Mratibu wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) Kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Bw, Salimu Mwinjaka amesema, ziara ya kutembelea Programu ya kuendeleza kilimo na uvuvi inayotekelezwa na IFAD na serikali imekuwa ya mafanikio sana.

“Tumetembelea maeneo ya uzalishaji wa Mwani tumeona mafanikio halikadhalika, Programu ya kuendeleza kilimo na Uvuvi inaangalia jinsi unavyoweza kutatua changamoto zitakazojitokeza,” alisema,

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.