Habari za Punde

Mfumo wa CBMS Waunganishwa na MUSE

Mtaalam wa Masuala ya Bajeti kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Edson Toto, akielezea maeneo yaliyoboreshwa kwenye Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS) wakati wa kikao kazi cha Mafunzo ya Mfumo huo, jijini Dodoma.
Baadhi ya Wadau na Maafisa kutoka Wizara ya Fedha wakiwa kwenye Mafunzo ya Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS) ulioboreshwa, unaofanyika jijini Dodoma.  

Wadau kutoka Wizara, Idara, Wakala wa Serikali na Mamlaka za Serikali za Mtaa, wakiwa katika Mafunzo ya Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS), jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)Na. Peter Haule, WF, Dodoma  

Wizara ya Fedha katika kusimamia maandalizi na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali, imefanya kikao kazi cha mafunzo ya Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS) ulioboreshwa uliounganishwa na Mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE) ili kurahisisha uingizaji wa takwimu za bajeti kwa mwaka 2024/25.

 

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Bajeti, Wizara ya Fedha, Bi. Bahati Mgongolwa, wakati akifungua mafunzo ya Mfumo huo kwa maafisa wanaohusika na masuala ya mipango na uingizaji wa takwimu za bajeti.

 

“Washiriki wamepitishwa kwenye mwongozo wa maandalizi ya Bajeti ya 2024/25 na maeneo ya Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS) yaliyoboreshwa ambapo baada ya mafunzo kukamilika mfumo utakuwa tayari kwa ajili ya kuanza zoezi la kuingiza maoteo ya bajeti ya mwaka 2024/25’’, alieleza Bi. Mgongolwa.

 

Alieleza kuwa miongoni mwa maboresho yaliyofanyika ni kuunganishwa kwa Mfumo wa CBMS na MUSE ili iweze kubadilishana taarifa za kibajeti zikiwemo za mapato na matumizi.

 

Bi. Mgongolwa, alisema maboresho hayo yatasaidia kutoa ridhaa ya matumizi kutoka Mfumo wa CBMS na kupeleka MUSE, kurahisisha uandaaji, uchambuzi na usimamizi wa bajeti pamoja na utoaji wa migao ya kila mwezi.

 

Vilevile alisema kuwa umewekwa utaratibu wa pamoja kwenye mifumo ya kibajeti na kiuhasibu kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za Government Finance Statistics (GFS), kurahisisha uandaaji wa mpango kazi na mtiririko wa matumizi kwa upande wa mapato na matumizi.

 

Bi. Mgongolwa alisema kuwa maboresho hayo yatasaidia ufanisi wa mfumo wa matumizi katika muda wa kati (MTEF) kwa kuboresha mifumo na taarifa ili ziwe na maoteo ya bajeti yanayoakisi ukweli katika muda wa kati.

 

Mafunzo ya Mfumo wa CBMS yamewashirikisha wadau kutoka Wizara, Idara, Wakala wa Serikali na Mamlaka za Serikali za Mtaa na yanatarajiwaa kuhitimishwa Desemba 21, 2023.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.