Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Akagua Mradi wa Maji,Hospitali ya Wilaya Rorya

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Rorya, Mhandisi James Kishinhi kuhusu pampu ya sasa iliyopo kwenye mradi wa maji wa Komuge uliyopo Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Februari 28, 2024.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua mradi wa maji wa Komuge uliyopo Wilaya ya Rorya mkoani Mara
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Rorya

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wilayani Rorya mkoani Mara, Februari 28, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Rorya waendelee kumuamini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kampeni yake ya kumtua mama ndoo kichwani.

“Rais wetu Dkt. Samia anataka muendelee kumuamini kwenye kampeni yake ya kumtua ndoo mama kichwani kwa kuwa amedhamiria kuwaletea maji katika maeneo yenu ili kila Mtanzania aweze kupata huduma ya maji safi na salama karibu na anapoishi.”

Amesema hayo leo (Jumatano, Februari 28, 2024) mara baada ya kukagua mradi wa maji wa Komuge uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, mkoani Mara.

“Mtulie, muwe na imani na Serikali yenu, muwe na uhakika na Serikali yenu. Na Serikali yenu iko imara na itaendelea kuwahudumia kwenye mambo yote ya msingi ambayo ni mahitaji ya kila siku ikiwemo afya, maji, barabara na elimu,” amesisitiza.

Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa Halmashauri zote nchini kuwa na utaratibu wa kufanya ziara kwenye maeneo yao ili wasikilize changamoto za wananchi na kuzifanyia kazi.

Akitoa taarifa za mradi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Rorya, Mhandisi James Kishinhi alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa tenki kubwa la maji kwani lililopo lina ujazo wa lita 225,000 na chujio la maji yanayovutwa kutoka ziwani.

Alisema wanahitaji sh. milioni 720 ili ziweze kutatua changamoto hizo ikiwemo kujenga tenki kubwa la lita 500,000 na pampu ya kusukumia maji kwenye vijiji 10 vinavyotegemea mradi huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema ili mradi wa maji uweze kukamilika unahitajika kuwa na chanzo, tenki la maji, eneo la kutibu maji na miundombinu ya usambazaji, ambavyo vyote vipo katika eneo hilo isipokuwa eneo la kutibu maji.

“Eneo la kutibu maji tutajenga, tenki lipo lakini halitoshelezi nalo tutajenga kubwa la lita 500,000 na sisi tunatambua kuwa maji ni muhimu na hayana mbadala. Maji si wali kusema ukiacha kuula utakula ugali, kwa hiyo ninamwagiza Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA alete sh. milioni 720 ndani ya wiki hii.”

“Hii kazi haihitaji kufanywa na mkandarasi, tutaifanya wenyewe ili ndani ya miezi mitatu mradi huu uwe umeisha,” alisisitiza.

Mapema, Mbunge wa Rorya, Jaffari Chege aliishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa chuo cha VETA ambacho tayari kimeanza kujengwa, gari la wagonjwa kwa Kituo cha Afya cha Kinesi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na mkakati wa kuboresha sekta ya afya nchini ili kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa hospitali ya wilaya ya Rorya, mkoani Mara, Mheshimiwa Majaliwa ameagiza kuendelea kukamilishwa kwa ujenzi wa hospitali hiyo pamoja na kununua vifaa tiba ili kuimarisha hali ya utoaji huduma kwa wananchi.

“Kukamilika kwa hospitali hii kutasaidia kupunguza gharama kwa wakazi wa maeneo ya karibu kutembea umbali mrefu hadi Tarime kufuata huduma za afya, hospitali hii ni suluhisho”.

Ujenzi wa hospitali hiyo ambayo inajengwa kwa njia ya force account umeshatumia kiasi cha sh. bilioni 3.25 kutoka Serikali kuu na mwaka 2020 ilianza kutoa huduma mbalimbali za wagonjwa wa nje ambapo inahudumia takribani watu 400 kwa mwezi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.