MKE wa Rais wa
Zanzibar, Mhe. Mama Mariam Mwinyi ameiasa jamii
kujitahidi kukithirisha ibada ndani ya mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan na kutoa
sadaka kwa wingi hasa kuwafikia watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo wazee,
watoto yatima, wenyeulemavu na masikini ili kupata radhi za Mwenyezi Mungu
(S.W).
Mama Mariam Mwinyi ambae
pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora
Foundation (ZMBF), aliyasema hayo kwa nyakati tofauti kwenye ziara yake
aliyowakilishwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Anna Athanas Paul alipowatembelea wazee wa Welezo na Sebleni, watoto yatima
waliopo Kijiji cha SOS na Mazizini, pamoja na kituo cha kulelea watoto
wanaoishi kwenye mazingira magumu, kilichopo Fuoni Mambosasa (ZASO), Mkoa wa
Mjini Magharibi ambako aliwasalimia, kuwafariji na kuwapa zawadi ya futari.
Alisema, ibada ya
sadaka sio lazima kutolewa zaidi kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, bali
hata siku za kawaida kwani zinaogeza upendo na kuigusa jamii yenye uhitaji.
“Kama kawaida desturi
yetu mwezi wa Ramadhan huwa tunatembeleana, kujuliana hali, sio desturi pekee
lakini pia ni maagizo kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, anatutaka waja wake
kutoa sadaka kwa wingi na kufanya zaidi mambo mazuri ya kumridhisha Yeye kama
kuwakumbuka wazee, wajane, watu wasiojiweza na masikini kuwapa sadaka ili nao
watekeleza vizuri ibada hii ya mwezi mtukufu wa Ramandani” Alisema Mama Mariam.
Mama Mariam alitumia
fursa hiyo kuwafikishia salamu za Rais wa Zanzibar na kuwaeleza kwamba yupo
pamoja nao wakati wote wa mfungo wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Alisema, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuyaenzi matunda ya Mapinduzi bado inaendelea
kuwajali na kuwaenzi wazee kwenye nyumba maalumu pamoja na watotoyatima ambao
Serikali inawaangalia kwa jicho la karibu.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti, Mkurugenzi wa Idara ya Ustawi wa Jamii na Wazee, Hassan
Ibrahim Suleiman na Mkurugenzi wa kituo cha kulelea watoto yatima SOS, Asha
Salum Ali waliishukuru ziara ya Mama Mariam kwenye taasisi hizo na kueleza
msaada alioutoa kwa wazee na watoto hao umewafikiwa wakati sahihi.
Walieleza, licha ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa huduma kama hizo kila mwezi katika
jitihada zake za kuwaenzi na kuwatunza watu wenye mahitaji maalum, pia msaada
huo alioutoa Mama Mariam Mwinyi utaongeza tija na kuwasaidi wakati huu wenye
uhitaji.
Pamoja na mambo
mengine Wakurugenzi hao pia walimuombea dua na mtakia kheir Mama Mariam Mwinyi kwa
jitihada zake anazozitoa kwa makudi maalum.
Pia, wakurugenzi hao
kwa niaba ya walenzi na wafanyakazi wa taasisi hizo walimuombea dua na makazi
mema peponi, Mwanzilishi wa kituo cha kulelea watoto yatima cha SOS, Marehemu
Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,
aliefariki hivi karibuni na kueleza msaada huo umekuja kama sadaka kwao.
Miongoni mwa msaada
waliopatiwa wazee na watoto hao ni pamoja na tende, vyakula vikiwemo mchele,
unga wa ngano, sembe, mafuta ya kupikia, sukari pamoja na vyakula vya nafaka.
IDARA YA MAWASILINO,
IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment