Habari za Punde

TigoZantel Yakabidhi Vibanda kwa Wafanyabiashara wa Miamala na Simu

MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa ameuagiza uongozi wa Baraza la Manispaa Mjini, kuhakikisha unaweka mazingira mazuri ya wafanyabiashara ili waweze kufanya biashara zao katika maeneo salama na ya kupendeza.

Kitwana alieleza hayo wakati akigawa vibanda kwa wafanyabiashara wa miamala na simu iliyotolewa na kampuni ya simu ya mkononi Tigo Zantel hafla iliyofanyika katika maeneo ya Darajani.

Alisema wapo baadhi ya wafanyabiashara miamvuli yao imechoka hivyo ni lazima jambo hilo kulitekeleza kama alivyoagiza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kuona wafanyabiashara wanawekewa mazingira mazuri ya biashara zao.

Aidha alisema hatua hiyo pia itasaidia kwa kiasi kikubwa kuweka mazingira mazuri na ya kupendeza katika mji wa Zanzibar ikizingatiwa eneo la Mji Mkongwe na Darajani limekuwa likitembelewa sana na wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani.

“Tengenezeni mazingira kuona mji unakuwa mzuri lakini watu wanafanya biashara zao vizuri na sitaki kusikia raamadhani huyu kachukuliwa mkungu wake wa ndizi,” alisema.

Aliipongeza kampuni ya Tigo Zantel kwa kuunga mkono agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alilolitoa hivi karibuni alipowatembelea wafanyabiashara kuwatengezea mazingira mazuri wafanyabiashara hasa wanaojishughulisha na mambo ya simu na miamala na hata wafanyabiashara wengine wanaofanya biashara zao Darajani na maeneo mengine ya Mji Mkongwe.

Mbali na hayo aliwasisitiza wafanyabiashara kufuata maelekezo wanayopewa ili kuondosha usumbufu unaoweza kujitokeza hasa kwa wananchi wanaofika katika eneo hilo kwa ajili ya kupata huduma.

Hata hivyo, aliwashauri wadau wengine kujitokeza kuitikia wito wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi wa kutengeneza mazingira mzuri ya wafanyabiashara katika mji wa Zanzibar.

Naye Mkurugenzi Tigo Zantel, Aziz Said Ali, alisema lengo la kutoa vibanda hivyo vya kisasa ni kuweka mazingira mzuri ya wafanyabiashara katika eneo hilo huku wakiunga mkono juhudi za Rais Mwinyi kuhakikisha wafanyabiashara hawakai ovyo pembezoni mwa barabara.

Alibainisha kuwa kwa kila eneo watakaoloruhusiwa kuweka vibanda hivyo kwa Darajani na Mji Mkongwe basi wataendelea kuyafanya hivyo ili kuona mji unavutia hasa kwa wageni.

Nao baadhi ya wafanyabiashara waliipongeza Tigo Zantel kuwapatia vibanda hivyo kwani awali walikuwa wanafanya biashara zao katika mazingira magumu na sio salama.

Wakala Ashura Ali alisema mwanzo walikuwa wanafanyabiashara lakini walikuwa wakipata shida ikiwemo kupata jua, kuungua na kukosa vitendea kazi lakini hivi sasa kupatiwa vibanda hivyo vimewawezesha kupata mazingira mazuri ya kufanyia kazi.

Naye Mfanyabiashara wa miamala ya simu Juma Abdalla Shafii, alimpongeza Rais Mwinyi kwa kauli yake aliyoitoa kuona wafanyabiashara wanaachiwa kufanya biashara zao ili kujiendeleza kiuchumi.

Hivyo, waliahidi kujipanga upya ili kuona wanatoa huduma nzuri kwa wateja wao katika mazingira mazuri na yakupendeza.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.