Habari za Punde

Waziri Mhe.Jafo Awasilisha Taarifa ya Miradi Kwenye Kamati ya Bunge

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Urejeshwaji wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) unaotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Wilaya Iringa pamoja na Mradi wa Hifadhi Endelevu ya Ardhi katika Bonde la Ziwa Nyasa (SLM-Nyasa) unaotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kilichofanyika jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema miradi mbalimbali ya mazingira imechangia kuwajengea wananchi uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ametoa kauli hiyo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Urejeshwaji wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) unaotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pamoja na taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Hifadhi Endelevu ya Ardhi katika Bonde la Ziwa Nyasa (SLM-Nyasa) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira katika kikao kilichofanyika leo Machi 12, 2024 jijini Dodoma.

Dkt. Jafo amesema kuwa kutokana na wananchi kuendelea kupata elimu ya mazingira, wameendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za upandaji wa miti hatua iliyochangia kupatikana kwa mvua katika maeneo mbalimbali nchini.

“Mheshimiwa Mwenyekiti kupitia Kamati yako mmefanya kazi kubwa sana kwani mmetupa maelekezo ambayo tumeyafanyia kazi hasa katika eneo la kuwaelimisha wananchi kuhusu kuhifadhi mazingira na matunda yake tunayaona, wananchi wengi wameendelea kupanda miti kwa wingi,” amesema.

Dkt. Jafo amesema kuwa kutokana na uharibifu wa mazingira katika bonde la Ziwa Nyasa unaotokana na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu, Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza Mradi wa SLM-Nyasa kuwajengea uwezo wananchi hao kutumia mbinu bora za kuhifadhi ardhi.

Ameongeza kuwa kupitia mradi huo wananchi wanaojengewa uwezo wanaweza kuboresha maisha yao kwa kuwa na njia mbadala ya kujipatia kipato na kuachana na vitendo vya ukataji wa miti ovyo au uvuvi usio endelevu.

Halikadhalika, Waziri Dkt. Jafo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza Mradi wa SLR ili kuimarisha usimamizi jumuishi wa mazingira na urejeshwaji wa mazingira yaliyoharibiwa ili kujenga uhimilivu wa mifumo ikolojia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.