Habari za Punde

DKT. KHALID AFUNGA MAFUNZO NA MASHINDANO YA WASICHANA NA TEHAMA

Na Takdir Ali. Maelezo. 30.04.2024.

Waziri wa ujenzi, mawasiliano na uchukuzi Dkt. Khalid Salum Mohamed amewataka waandaaji wa mafunzo mbalimbali kuwa na takwimu maalum ili wawaeze kuwafuatilia, kuwawezesha na kuwaunganisha katika soko la ajira.


Ameyasema hayo huko katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip uwanja wa ndege katika hafla ya kufunga mafunzo na mashindano ya wasichana na TEHAMA katika kituo cha Zanzibar.


Amesema kuna mafunzo mengi yanayotolewa lakini yamekuwa hayafikii malengo kutokana na waandaaji kutowapa msukumo na kuwaacha mkono jambo ambalo ni kupoteza muda na rasilimali.


“Lazima mawasiliano yawe chaju ya mabadiliko katika maendeleo kwani bila kuwepo mabadiliko ni hatari na tutaendelea kufanya kazi kwa mazoea.” Alisema Dkt. Khalid.


Aidha amezishauri taasisi husika kuweka mikakati itakayoyawezesha matokeo ya mafunzo hayo,yaweze kuchangia na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.


“Zanzibar asilimia kubwa ya mawasiliano inatumika kwa mambo maovu, tuchukulie mfano matumizi ya simu, watu wanatumia simu kwa ajili ya kuchati na mipasho jambo ambalo halisaidii lolote katika maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.” Alisema Waziri huyo.


Pia amewataka Wanafunzi kuitumia vizuri elimu hiyo kwa kufanya mambo yatakayowasaidia katika kuleta maendeleo na sio kufanya mambo ya kipuuzi.


Mbali na hayo amewataka Wanawake wasiogope kusoma masomo ya sayansi kwani Serikali zote mbili zinatilia mkazo wanawake kusoma masuala ya sayansi na teknolojia.


Sambamba na hayo ameutaka mfuko wa mawasiliano kwa wote (USCAF) kuwaangalia uwezekano wa kuwashirikisha na wanafunzi wa kiume ili waweze kushirikiana na wasichana na kuweza kufikia malengo yaliokusudiwa.


Mbali na hayo amesema Serikali imeweka mpango maalum ya madarasa ya tehama ili kuhakikisha hakuna anaeachwa nyuma katika mageuzi ya kiditali na kuwaomba kuitumia vizuri fursa hiyo ili waweze kuendana na wakati uliopo wa sayansi na teknolojia.


"Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi ameagiza Skuli zote za Sekondari ziunganishwe na mkonga wa taifa ili wanafunzi waweze kusoma na kuwarahisishia kupata huduma.” Alibainisha Waziri huyo.


Kwa uapnde wake Katibu mkuu wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dkt. Mngereza M. Miraji ameupongeza mfuko wa Mawasiliano kwa wote kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yanasaidia kutekeleza mikakati iliowekwa na Serikali zote mbili katika kusomesha masomo ya Tehama.


Hata hivyo amesema Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ipo katika mifumo ya Tehama hivyo mafunzo hayo yatakuwa chachu na mabadiliko katika utendaji na kudhibiti mapato ya Serikali.


Mapema akitoa maelezo afis mtendaji mkuu wa Mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) Bi Jostina Mashiba amesema wameamua kuandaa mafunzo hayo baada ya kubaini Watoto wengi wa kike wanakimbia kusoma masomo ya Tehama.


Aidha amesema katika kuhamasisha na kuunga mkono wasichana hao wamekabidhi Compyuta na Vifaa vya UCSAF ili waweze kujuwa na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kuwaunga mkono na kuweza kukamilisha malengo yaliopangwa.


Jumla ya wasichana 248 kutoka mikoa yote 31, wameshiri katika mafunzo hayo na 57 walifanya mafunzo kituo cha DIT Cumpus ya Mwanza, ATC wanafunzi 31, Veta Dodoma wanafunzi 40, Veta Mbeya wanafunzi 40, COSTECH Dar es salaam wanafunzi 40 na kituo cha Tehama Bwefum Zanzibar Unguja na Pemba Wanafunzi 40.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.