Nchi
wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Southern African
Development Community-SADC) zimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ,Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake katika usimamizi na
uhifadhi wa misitu miombo hasa katika kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati chafu
kuelekea nishati safi ifikapo mwaka 2030.
Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 18,2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) katika Mkutano wa Kimataifa unaohusu Misitu ya Miombo jijini Washington DC nchini Marekani.
“Kikubwa nchi zimeweza kumpongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akitoa maelekezo mbalimbali kwetu sisi kama Wizara na Sekta katika kuhakikisha kwamba misitu ya miombo inalindwa kwa nguvu kubwa, na kwa namna ambavyo amechukua uamuzi thabiti wa kuhakikisha kwamba inapofika mwaka 2030 zaidi ya asilimia 80 ya wananchi watakuwa wameachana na matumizi wa kuni na mkaa na watakuwa wamejielekeza katika nishati safi ya kupikia” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Amesema kuwa misitu ya miombo nchini Tanzania katika ukanda wa kusini imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uharibifu wa misitu ikiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji, ukataji miti hovyo lakini Rais Samia amekuwa na jitihada mbalimbali kama Taifa kuhakikisha inalindwa kwa nguvu kubwa.
Aidha, amefafanua kuwa kupitia mkutano huo, nchi za SADC zimeweza kupata wafadhili ambao wameanza kuonesha nia ya kusaidia mpango wa utekelezaji wa Azimio la Maputo la mwaka 2022 kuhusu ulinzi na uendelezaji wa misitu ya miombo.
Amesema lengo la Mkutano huo ni kuona namna ya kuendeleza Azimio la Maputo katika kulinda na kuendeleza Misitu ya Miombo ambapo Tanzania ina zaidi ya asilimia 93 ni Misitu hiyo yenye aina ya spishes zaidi ya 8500, inatunza wanyamapori , miti na ina faida za kiuchumi na kijamii kwa upande wa masuala ya kilimo, upatikanaji wa dawa, chakula , vyanzo vya maji na huduma nyingine za msingi
Naye, Kamishna Uhifadhi wa
Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo amesema kuwa kupitia mkutano huo nchi za SADC
zimekuwa na majadiliano kuhusu kutafuta namna ya kushirikiana baina ya nchi hizo na wadau mbalimbali wa maendeleo
katika kupata rasilimali fedha, na kukuza ujuzi na utaalamu kwa ajili ya
kuaidia uhifadhi wa misitu hiyo.
Amoengeza kuwa kongamano hilo limehitimishwa na hotuba ya Rais w Jamhuri ya Watu wa Msumbiji, Mhe.Filipe Jaciton Nyusi ambapo amesisitiza umuhimu wa nchi hizo kushirikiana katika kubadilishana taarifa , kukabiliana na masuala ya uharibifu wa mifumo ya ikolojia ya miombo hususan biashara haramu za mazao ya misitu na wanyamapori katika ukanda wa SADC.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Idara ya Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Deusdedith
Bwoyo amesema kuwa mkutano huo ni muhimu sana wa kuweza kuzungumza kwa pamoja
changamoto za misitu ya miombo kwa nchi wanachama 11 za ukanda wa SADC na
umekuja na majibu ya kuendeleza misitu ya miombo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (kulia) akiwa na baadhi ya Mawaziri wa nchi za SADC katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo jijini Washington DC nchini Marekani leo Aprili 18,2024.
Rais wa Jamhuri ya Watu wa Msumbiji, Mhe.Filipe Jaciton Nyusi (wa tatu kutoka kulia) katika picha ya pamoja na Mawaziri wawakilishi kutoka nchi za SADC walioshiriki Mkutano wa Kimataifa kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo jijini Washington DC nchini Marekani leo Aprili 18,2024. Kushoto kwake ni Waziri wa Ardhi na Mazingira wa Msumbiji, Mhe.Ivete Maibaze na Balozi wa Umoja wa Afrika nchini Marekani, Mhe. Hilda Suka-Mafdze (kulia). Katikati ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb).
No comments:
Post a Comment