RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi ameihakikishia Serikali ya Saudi Arabia ushirikiano mzuri uliopo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa kwenye miradi mbalimbali ya Maendeleo.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na Balozi
wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Mhe. Yahya Ahmad Okeish
na ujumbe wake kwa lengo la kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya nchi mbili
hizo.
Dk. Mwinyi alisema, SMZ ni mnufaika mkubwa wa mfuko wa Saudia na
Quwait kwenye miradi yake ya maeneleo kupitia ushirikiano mzuri uliopo baina ya
mataifa hayo.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameishukuru na kuipongeza Serikali ya
Saudi Arabia kwa ushirikiano wake na Tanzania hususan kuipatia Zanzibar zawadi
mbalimbali inazozituma kwa watu wa Zanzibar ikiwemo tende wakati wa Mwezi
mtukufu wa Ramadhan.
Katika salamu zake kwa Tanzania, Balozi Okeish amepongeza
mafanikio makubwa yaliyofikiwa na taifa hili kwa kutimiza miaka 60 ya Muungano
wake baina ya Tanganyika na Zanzibar sambamba na kuuombea mafanikio zaidi
muungano huo.
Pia, Balozi Okeish alisifu ushirikiano wa diplomasia uliopo
baina ya Saudi Arabia na Tanzania ikiwemo Zanzibar pamoja na kusifu tamaduni za
pande mbili hizo.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment