Habari za Punde

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibare Mhe.OthmanMasoud Atembelea Mashamba ya Chumvi Kijiji cha Shengejuu Pemba

 

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman ,amesema kwamba wazalishaji wa Chumvi wa Kijiji cha Shengejuu wilaya ya Wete wanayo fursa kubwa ya kujikwamua na umasikini iwapo watasaidiwa ili waweze kuzalisha kitaalamu na kuweza  kuongeza thamani na kupata tija zaidi ya wanachozalisha.

Mhe. Othman ameyasema hayo alipotembelea Mashamba ya ushirika wa wazalishaji Chumvi wa Kijiji cha Shengejuu wilaya ya wete Kisiwani Pemba alipofika kuona hali halisi ya changamoto zilizopo kwenye eneo hilo zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi na vitendo vya binaadamu vinavyosababisha uharibifu wa mazingira.

Amefahamisha kwamba eneo hilo nimuhimu na limechukuwa idadi kuwa ya wananchi waliojiajiri, lakini mbali ya kuwa na changamoto ya barabara   na miundombinu mingine inayotumika hapo pia suala la mabadiliko ya tabia nchi nalo limeathiri sana uzalishaji wa chumvi katika eneo hilo na kupungunza matumaini ya wazalishaji hao.

Amefahamisha kwamba kutokana na hali hiyo na kwakuwa suala la mabadiliko ya tabia nchi linasimamiwa na ofisi yake, serikali itapeleka wataalamu wake kwenda kuona na kufanya tathimini ili kuja na mpango sahihi wa kusaidia kunusuru hali katika eneo hilo na wazalishaji waweze kuendelea na shughuli zao ikiwa ni pamoja na kuibua fursa zaidi kwenye eneo hilo.

Hivi sasa katika eneo hilo lenye idadi kubwa ya wajasiriamali wanaozalisha chumvi,  kingo nyingi za mashamba yanayotumika kuzalisha chumvi yameharibika vibaya miundombinu yake kutokana na kingo za mashamba hayo kupasuka kulikosababishwa  na ongezeko la kasi ya maji jambo ambalo linaathiri uzalishaji huo.

Mhe. Makamu amesema kwamba hatua ya kupeleka wataalamu itasaidia kufanya tathimini ili kuja na mikakati bora na kuandaliwa mpango madhubuti utakaotumika kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na matendo ya wanaadamu ndani ya eneo hilo.

Amesema kwamba tatizo la tabia nchi ni la kidunia ambapo sehemu kubwa ya hali hiyo inatokana na nchi tajiri zenye viwanda vikubwa duniani na shughuli zao za uzalishaji viwandani zinaongeza joto duniani na hali hiyo  imechangia sana barafu iliyopo katika sehemu tofauti kuyayuka na kusababisha kina cha maji kuongezeka, lakini waathirika wakubwa ni nchi masikini ikiwemo Zanzibar.

Hata hivyo , Mhe. Othman amefahamisha kwamba hivi sasa serikali kupitia Ofisi yake ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuirejesha Zanzibar kuwa ya kijani na kwamba wananchi hao pia watapewa fursa ya kushiriki katika suala la upandaji miti pamoja na kuanzisha vitalu vya miti ili kutoa mchango wao wa kuirejesha Zanzibar kuwa ya kijani.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakari amesema kwamba  pamoja na kuwepo changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi ,lakini matendo ya binaadamu nayo yamechangia sana katika kuharibika  maeneo mbali mbali likiwemo hilo na kusababisha athari kubwa kwa kuongezeka maji yanayosambaa zaidi katika mashamba ya ukulima wa chumvi.

Amesema kwamba kuna haja ya wananchi kubadilika  hasa katika suala la ukataji wa miti ovyo kutokana na ukweli kwamba matendo ya namna hiyo nayo ndio chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wao wakulima wa chumvi katika eneo hilo walimueleza Mhe. Makamu kwamba licha ya jitihada kubwa wanazofanya kujenga matuta ya kuzuia maji hayo yasiathiri mashamba yao, lakini kutokana na nguvu  kubwa ya maji inayoongezeka kila siku uzalishaji huo umeshuka kwa kuwa maeneo mengine hayawezi kuendelea kutumika na  hawana uwezo wa kifedha kuendelea kurejesha miundombinu ya mashamba hayo.

Mhe. Othman yupo ziarani kisiwani Pemba kwa ziara ya chama na serikali na amefika katika eneo hilo la mashamba ya chumvi kuona hali halisi ya uharibifu wa mazingira kutokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuitathimini hali ili serikali iweze kupanga  mikakati na hatua stahiki za kuchukuliwa kunusuru hali hiyo isendelee kuleta madhara zaidi.

Mwisho.

Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Kupitia Kitengo chake cha habari leo tarehe 21.05.04.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.