Habari za Punde

Zanzibar inazofursa nyingi za kuweza kupiga hatua za kimaendeleo ya kiuchumi na wananchi

 Na.Mwandishi OMKR Pemba.

Mwenyekiti wa Chama cha ACT – Taifa Mhe. Othmani Masoud Othman, amesema kwamba chama hicho kinaamini kwamba Zanzibar  inazofursa nyingi za kuweza kupiga hatua za kimaendeleo ya kiuchumi na wananchi kuondokana na umasikini kinachohitajika ni uongozi wenye maono kama inavyotokea kwa nchi nyengine duniani.

Mhe. Othman Masoud ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameyasema hayo huko  Ukumbi wa Dolphini Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba alipokutana na viongozi wa Chama hicho wa Wilaya za Wete na Micheweni Kichama akiwa katika muendelezo wa ziara yake ya kukutana na viongozi wa chama hicho ngazi ya mikoa, wilaya na matawi.

Amesema kwamba viongozi wenye maono, uwezo wa kujitoa na kujitolea watakoweza kupanga na kutekeleza mikakati sahihi hya kiuchumi na kimaendelea kutaweza kuisaidia nchi kupiga hatua kwa kuzitumia fursa na rasilimali za nchi na wananchi kuweza kuongeza kipato kikubwa na kupambana na umasikini.

Amefahamisha kwamba zipo nchi mbali mbali duania ambazo zilikuwa na uwezo duni katika kipindi cha miaka ya nyuma lakini viongozi wake walitumia juhudi , maono na uwezo wako na hivyo kuweza kuzibadili nchi zao kiuchumi na kimaendeleo jambo amalo linawezekana pia kwa Zanzibar.

Aidha amesema kwamba katika kufikia ndoto za namna hiyo  viongozi ni lazima kuwa wa kweli na wenye kuwa na mamlaka na uwezo wa kupanga na kutekeleza mikakati mbali mbali  ya kiuchumi ambayo itaweza kupambana na hali ya umasikini na kuwasiadia wananchi kuweza kupiga hatua.

Amesema kwamba hali ilivyo sasa ya ukali wa maisha kwa wananchi inapelekea kuwepo baadhi ya watu kuwa na  fikra na matamshi ya kujutia kuzaliwa Zanzibar badala ya kujinasibu na uzanzibari wao.

Amewataka wanacnhi kuungana na chama hicho ambacho kimejimbambanua kwamba kinawajibu , uwezo na malengo ya kupigania haki za Zanzibar ndani ya muungano jambo ambalo haliwezi kufanywa na  Vyama vyengine.

Alisema kwamba maendeleo ya kweli ndani ya nchi kamwe hayataletwa kwa ihsani ya mataifa ama mtu yoyote, bali yatapatikana kutokana na juhudi za kweli kati ya wananchi na viongozi kwa kutumia rasilimali zao wenyewe.

Akizungunzia suala la serikali ya Umoja wa Kitaifa amesema kwamba chama chake kinaendelea kutumia hekima baada ya kufanya mazungunzo na viongozi wakuu lakini tayari kimeshafanya maamuzi ya kujitoa iwapo mambo ya msingi waliyokubaliana hayatatekelezwa .

Aliyataja masuala hayo kwamba ni pamoja na kuondoshwa kura ya mapema , kufanyiwa marekebisho mfumo wa uchaguzi pamoja na sekteratieti ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar pamoja na suala la wananchi kunyiwa vitambulisho vya uzanzibari Mkaazi.

Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa Chama hicho Ismail Jussa Ladhu amewaomba viongozi na wananchama wa chama hicho kutoyasahau malengo na dhamira ya chama chao kwa kufikiria kupata vyeo vya uwakilishi na ubunge.

Amsefahamisha kwamba masuala hayo sio lengo la chama na kufanya hivyo kwa njia ya tamaa ni kuleta mgawanyiko ndani ya chama na kwamba watakaobainika kuendelea na malengo hao chama hakitawaunga mkono kwa kuwa sio malengo yao.

Amesema masuala yote yanayoleta mgawanyiko ni kuharibu chama hicho na kwamba ni miongoni mwa masuala ambayo chama hakiweza kuyapa nafasi kuendelea kufanywa na watu wenye taama na uchu wa kupata vyema kwa kuwa waasisi wa chama hicho walijitolea  na kuacha vyeo vikubwa walivyokuwa navyo kwa kuzingatia kuweka mbele maslahi ya nchi na kuweka mbele uzalendo.

Mwenyekiti huyo wa ACT- yupo kisiwani Pemba kukutana na viongozi wa chama hicho ngazi ya matawi , majimbo , wilaya na mikoa ikiwa ni hatua ya kutoa shukrani  ya kuchaguliwa kwa nafasi hizo katika uchaguzi mkuu wa chama uliofanyika Mwezi Machi mwaka huu huko mjini Dar es Salaam.

Mwisho.

Imetolewa na ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia kitengo chake cha habari leo Jumanne tarehe 30.04.2024. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.