Habari za Punde

Siti Amekutana na Masheha Kujadili Ukatili na Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto Wilaya ya Kati Unguja

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Siti Abasi Ali akizungumza na Masheha wa Wilaya ya Kati kuhusiana na mikakati ya kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na Watoto, huko Dunga Mkoa wa Kusini Unguja.
Katibu wa Masheha Wilaya ya Kati Zidi Suleiman Abjeid akichangia katika kikao cha kujadili mikakati ya kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na Watoto, huko Dunga Mkoa wa Kusini Unguja.
Sheha wa Shehia ya  Bambi Amour Pandu Mkombe akichangia katika kikao cha kujadili mikakati ya kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na Watoto, huko Dunga Mkoa wa Kusini Unguja.


Na.Takdir Ali. Maelezo. 14.06.2024.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Siti Abasi Ali amewaomba Masheha wa Wilaya ya Kati kuwatafuta wamiliki wa Maboma ya nyumba na nyumba za kukodisha katika Shehia  zao ili kuziba myanya ya  vitendo viovu katika jamii .

Ameyasema hayo huko Dunga Wilaya ya Kati wakati alipokuwa akizungumza na Masheha hao pamoja na kujadili mbinu mbalimbali, zitakazoweza kuondosha vitendo hivyo na Watoto  kubaki salama mitaani.

Amesema baadhi ya majengo hayo katika  Shehia  hizo yamekuwa yakitumika  kufanyia vitendo hivyo vinavyoathiri jamii.

“ni vyema kuendelea kushirikiana kuweka mikakati ya kuondosha viashiria vinavyosababisha masuala ya udhalilishaji ili kuwakinga Wanawake na Watoto kutokana na viendo hivyo.”alisisitiza mkurugenzi Siti

Aidha amewataka masheha hao kushirikiana kikamilifu na  Waratibu wa jinsia katika shehia zao   ili malengo yaliopangwa na Serikali ya kupiga vita vitendo vya udhalilishaji yaweze kufikiwa.

“Nataka niwapongeze kwa dhati Waheshimiwa Masheha, munafanya kazi kubwa na ngumu lakini tunakuombeni muzidishe mashirikano na Waratibu wetu kwani tumewapa mafunzo ya kutosha na wanaleta ripoti kila baada ya miezi mitatu.” Alisema Mkurugenzi Siti.

Mbali na hayo Siti amewaomba Masheha hao kusimamia kuanzishwa Majukwaa ya Wanawake Wajasiriamali katika Shehia zao ili waweze kupata fursa mbalimbali zilizopo ikiwemo Mikopo.

Kwa uapande wake Katibu wa Masheha wa Wilaya ya Kati Zidi Suleiman Abjeid amesema wataendelea kutoa  ushirikiano wa kutosha kwa Waratibu hao licha ya  kazi ngumu wanayoifanya usiku na mchana.

Hata hivyo ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo waliopewa na Mkurugenzi huyo ili kuondoa  Janga la udhalilishaji kwa faida ya jamii  na Taifa kwa ujumla.

Nao baadhi ya Masheha wa Shehia za Wilaya ya Kati wameomba kutatuliwa changamoto zinazowakabili  ikiwemo kupatiwa posho la usafiri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.