SERIKALI ya
Mapinduzi ya Zanzibar imesema hatua ya kuanzisha bima ya afya kwa watalii
inalenga kuimarisha sekta ya utalii pamoja na kuandaa mazingira salama na
rafiki kwa wageni wanaokuja nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo
Ikulu, Zanzibar alipozungumza na balozi mpya wa Italia nchini, Giuseppe Sean Coppola
aliyefika kujitambulisha.
Dk. Mwinyi amesema bima ya afya kwa watalii sio
jambo geni kwani mataifa mengi duniani tayari wamekuwa na huduma hiyo ambayo
kwa kiasi kikubwa inamjengea mtalii uhakika wa kupata huduma bora za afya,
ulinzi wa ustawi wake ikiwemo kumuondoshea usumbufu anapopata tatizo lolote kama
kupoteza mizigo yake au hati za kusafiria.
Amefafanua kwamba Serikali imekua ikibeba mzigo
mkubwa wa gharama kwa wageni wanaongia nchini hasa wanapopata matatizo ya
ugonjwa, ajali wakati mwengine vifo, hivyo ameeleza kuanzishwa kwa bima hiyo
kutaipa Serikali unafuu.
“Sio nia ya Serikali kutafuta njia nyengine ya
kujiongezea mapato, bali ni namna bora ya kuiboresha sekta ya Utalii na
kuifanya Zanzibar kuwa kituo Salama kwa watalii wanaoingia nchini” Alifahamisha
Dk. Mwinyi.
Dk. Mwinyi amesifu ushirikiano uliopo baina ya
Zanzibar na Italia katika nyanja mbalimbali na kuisisitiza nchi hiyo kuunga mkono
juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hususan usimamizi bora wa taka kwa
kuziongezea thamani kuwa malighafi, afya na usalama wa bahari.
Akiizungumzia sekta ya Utalii, Rais Dk. Mwinyi
ameielezea Itali kuwa mdau mkubwa kwa maendeleo ya utalii wa Zanzibar kwani
imekua ikipokea idadi kubwa ya wageni kutoka nchini humo, hivyo amezialika
kampuni za uwekezaji kutoka Itali kuja kuwekeza Zanzibar kwenye sekta nyengine.
Naye, Balozi Sean Coppola
amemuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kushirikiana zaidi maeneo ya afya, utalii,
usimamizi wa taka kwa kuzichakata na kuwa rasilimali zenye tija pamoja na
maendeleo ya Uchumi wa Buluu ambao kwa Zanzibar umekua ni miongoni mwa sera kuu
ya Uchumi.
Kuhusu afya balozi Coppola amesema
watashirikiana zaidi hasa kwa maradhi yasiyopewa kipaumbele (NTDs) hususan
kisiwani Pemba pamoja na masuala ya afya ya mama na mtoto.
Akiielezea Sekta ya Utalii,
balozi huyo amesema, wataungamkono kwenye kuwajengea uwezo, vyuo vya utalii,
wadau na watendaji wa sekta hiyo, kwa mafunzo ya muda mfupi na mrefu lengo ni
kuifanya Zanzibar kuwa kituo bora cha utalii kinachotambulika duniani.
Balozi Giuseppe Sean
Coppola, aliwasilisha nakala ya barua za utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahmoud
Thabit Kombo, Ogasti 05 mwaka huu.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment