Na Happiness Shayo - Dar es Salaam
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Giuseppe Sean Coppola ambapo pamoja na mambo mengine wamekubaliana kushirikiana kwenye nyanja mbalimbali za Sekta ya Maliasili na Utalii.
Kikao hicho kimefanyika leo Novemba 18,2024 katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Chana amesema kuwa Tanzania na Italia zinaweza kuimarisha mashirikiano ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini huku akisisitiza kuwa ukuaji wa Sekta ya Maliasili na Utalii nchini unatokana na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii hasa kupitia filamu za “Tanzania The Royal Tour” na “Amazing Tanzania”.
"Tuimarishe ushirikiano katika Taasisi zetu za Sekta ya Maliasili na Utalii kati ya Tanzania na Italia katika utangazaji utalii , kufanya tafiti kujua Watalii kutoka Italia wanapenda nini, kubadilishana uzoefu katika ukarimu na uandaaji wa vyakula vya kiitaliano" Mhe. Chana amesema.
Naye, Mhe. Coppola amesema kuwa Italia iko tayari kushirikiana na Tanzania hasa kwenye maeneo ambayo yako katika mpango wa muda mrefu ikiwemo kujengeana uwezo wa mafunzo, kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Italia hadi Arusha na kutangaza vivutio vya utalii.
"Ninafurahishwa namna mnavyosimamia sekta hii ya Maliasili na Utalii na kwa sasa tunashirikiana na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) ambapo tunatarajia kusaini Hati ya Makubaliano na Mashirikiano na kati yake na Chuo cha Mafunzo ya Ukarimu cha Italia lengo ikiwa ni kujengeana uwezo kwenye Ukarimu, Utafiti kwa pamoja na kubadilishana uzoefu kati ya wanafunzi na walimu baina ya nchi hizo mbili.
No comments:
Post a Comment