Na.Kitengo cha Habari OMKR .
Mwenyekiti wa Chama cha ACT wazalendo Taifa Mhe. Othman Masoud Othman, amewataka wanachama wa Chama hicho pamoja na wananchi kwa jumla kusimama pamoja katika kupigania mageuzi ya kisiasa Zanzibar jambo litakalosaidia kuondoa kero na matatizo ya wananchi waliyonayo.
Mhe. Othman
ameyasema hayo huko katika Kijiji cha Muwi Shehia ya Mjanaza Jimbo la Pandani wilaya ya Wete Kaskazini
Pemba alipojibu hoja mbali mbali za wanakijiji hao baada ya kuwapa fursa ya
kuuliza maswali alipowatembelea kijijini
hapo akiwa kwenye ziara ya Kisiasa na
Kiserikali kisiwani Pemba.
Amesema
kwamba chama hicho kimejipambanua kutetea mabadiliko na mageuzi ya kisiasa
nchini kutokana na wananchi wengi kuwa na
kero mbali mbali zikiwemo za huduma za kijamii wanazostahiki kuzipata bila
kuwepo usumbufu wowote.
Amefahamisha
kwamba zipo huduma nyingi kama zile vyeti vya Kuzaliwa na Kitambulisho cha
Mzanzibari mkaazi ambazo ni miongoni mwa
zilizowekwa rasmi na Serikali na wananchi wote wanastahiki kuzipata bila kuwepo
usumbufu jambo ambalo ni kinyume na ilivyo sasa.
Amesema
kwamba viongozi wengi wameapa viapo vya uaminifu kulinda Sheria na Katiba
kutokana na dhamana zao walizopewa lakini wengi wanavikiuka viapo hivyo kwa
kuviendea kinyume na pia kutozingatia matakwa ya sheria ikiwemo sheria mama
ambayo ni Katiba.
Amefahamisha
kwamba ni muhimu kwa viongozi wa serikali na watumishi wengine wa umma kuhakikisha
kwamba wanawajibika kwa wananchi kwa kuwatumikia kwa mujibu wa sheria na viapo
vyao kwa kuwa kufanya hivyo ndio wajibu wao kwa wananchi na ni matakwa ya sheria
na katiba ya Zanzibar.
Amesema
kwamba viongozi wengi wamekuwa majasiri wa kuropoka kwa kutetea masuala ambayo
kisingi ni batili na yanakwenda kinyume na matakwa ya sheria na katiba ya nchi
jambo ambalo linahitaji kuondolewa kupitia kura za wananchi na kuleta mageuzi .
Aidha
amesema kwamba suala hilo pia ni muhimu katika kurejesha nidhamu ya serikali
kwa kuwa na viongozi waliochaguliwa na wananchi wanaowajibika kwao katika
kupigania maslahi ya kimaendeleo katika taifa lao.
Mapema
baadhi ya wananchi wa Jimbo la pandani kutoka shehia za Mjananza, Mlindo, Muwi
na nyenginezo walilamika mbele ya Mhe. Othman kwamba wamekuwa wakipta usumbufu
mkubwa wa katika kupatiwa huduma za vitambuliso vya mzanzibari mkaazi pamoja na
vyeti vya kuzaliwa.
Mhe. Othman
anaendelea na ziara yake ya siasa na Kiserikali kisiwani Pemba na Kesho tarehe
3 Disemba 2024 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya
siku ya watu wenye ulemavu duniani ambapo kwa Zanzibar yanatarajiwa kufanyika
katika viwanja vya Gombani ya Kale wilaya ya Chake chake mkoa wa Kusini Pemba.
Mwisho
Imetolewa
na ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzib ar kupitia Kitengo chake cha
Habari leo Disemba 2, 2024.
No comments:
Post a Comment