SERIKALI
ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kuungamkono juhudi za Muhimili wa Mahkama
zenye lengo la kuleta mageuzi makubwa katika miundombinu ya majengo ya Mahkama.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ametoa tamko hilo alipoweka jiwe la
msingi la ujenzi wa Mahkama ya Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ameeleza, Serikali ya imefanikiwa kuleta mageuzi makubwa kwenye majengo
ya Mahkama kwa kutowa fedha za ndani kwa asilimia mia jambo alilolieleza kuwa
la kujivunia.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameeleza mageuzi hayo yana lengo la kutoa huduma
bora kwa wananchi katika mazingira yakuridhisha hatua aliyoielezea kwamba
itaijengea heshima muhimili huo.
“Tumetumia fedha zetu wenyewe kwasababu tungetumia wafadhili tungechelewa
kufikia mafanikio haya” alibainisha Rais Dk. Mwinyi.
Akilizungumzia jengo la zamani la Mahkama ya Vuga, Rais Dk. Mwinyi
ameeleza litaendelea kuwa la Mahkama na kuridhia azma ya Mahkama ya kulifanya
jengo hilo kuwa makumbusho ya Mahkama.
Pia, Rais Dk. Mwinyi amebainisha kuwa kwa miaka mingi muhimili huo
umekuwa ukitekeleza majukumu yake kwenye hali ya uchakavu wa majengo yake.
Amefahamisha kuwa, palipo na majengo mazuri lazima huduma bora zipatikane
hivyo, alieleza kuridhishwa kwake na mabadiliko makubwa ya utendaji wa Mahkama
hivi sasa. Sambamba na kueleza kuwa Mahkama inakusudia kujenga jengo jengine
kubwa litakalokuwa na Mahkama ya Rushwa na Uhujumu wa Uchumi.
Vile vile, amebainisha majengo mengine yatakayojengwa na mahkama hiyo kwa
nguvu wa Serikali ni pamoja na Mahkama ya Wilaya Makunduchi, jengo la Wilaya ya
Magharibi A Kijichi, Mahkama ya watoto Mahonda na Mahkama ya Wilaya ya Wete,
Pemba na kueleza kuwa majengo yote hayo mapya yatakuwa na huduma za teknolojia
ya kisasa.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan
Shaaban ameipongeza Serikali ya awamu ya nane kwa urahisi wa kupatikana fedha
uliofanikisha mahkama kujenga jengo hilo kwa muda mfupi sana.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Mahkama, Kai Bashir Mbarouk ameeleza mageuzi ya
majengo yanayofanyika hivi sasa, yanalengo la upatikanaji wa haki kwa wakati na
kuondosha malalamiko kwa wananchi wanaofika Mahakamani hapo kusikiliza kesi
zao.
Amefahamisha ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 85 ili ukamilike,
ambao utajumuisha huduma zote Mahkama.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment