RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi,
ameiagiza Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kuandaa mkakati
maalum utakaovutia na kuleta mashindano ya michezo mbalimbali nchini ili viwanja
vilivyojengwa kutumika ipasavyo.
Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipozindua awamu ya pili ya
Uwanja wa “Amani Sports Complex,” Mkoa wa Mjini Magharibi, uliojumuisha miradi mbalimbali ikiwemo hoteli
inayokaribiana na hadhi ya nyota tano, mkahawa wenye hadhi ya kimataifa,
maegesho ya magari, maduka na viwanja mbalimbali vya michezo (In door games) ya
Judo, Ngumi, mpira wa kikapu (basketi
ball), mpira wa wavu, (volleyball), mpira wa mikono (hand ball) na mchezo wa “long
tennis”, ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra
za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Ni lazima kuandaa mashindano makubwa
ili viwanja hivi kutumika ipasavyo” alisisitiza, Rais Dk. Mwinyi.
Pia, Rais Dk. Mwinyi amehimiza kutumiwa
kwa kumbi za mikutano zilizomo kwenye uwanja wa huo kwa mikutano ya ndani na ya
kimataifa pamoja na kutoa wito kwa wananchi kuzitumia fursa zinazopatikana
viwanjani hapo kwa kushiriki michezo hiyo kwa lengo la kujiongezea tija na
kukuza sekta ya michezo nchini.
Dk. Mwinyi ameeleza kuwa Zanzibar ina
kila sababu ya kujivunia kwa kuwa na viwanja bora vyenye viwango vya kisasa vya
kimataifa.
Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar awamu ya nane imeiweka Zanzibar kwenye viwango vya kimataifa, hasa
linapokuja suala la michezo kwamba itazidi kujibebea hadhi ya kimataifa kwa kuwa
na viwanja vyenye hadhi ya juu kila eneo.
Akizungumzia michuano ya AFCON ambapo Tanzania wa kushirikiana
na Kenya na Uganda wanatarajiwa kuwa wenyeji wa mashindano hayo, Rais Dk.
Mwinyi ameeleza kuwa Zanzibar ikiwa Sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
imejiandaa kwa mashindano hayo kwa kujenga miundominu yenye hadhi ya kimataifa
kama mwenyeji wa mashindano hayo.
Amesema, kuelekea AFCON Zanzibar itaunda kamati maalum ya
kitaifa itakayosimamia michuano hiyo kwa mafanikio makubwa.
Hafla ya uzinduzi wa awamu ya pili ya Uwanja wa “Amani Sports Complex,” iliambatana na Sherehe maalum
ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Mhe. Rais Dk. Mwinyi iliyoenda sambamba na
ukataji wa keki na wimbo maalum wa kumpongeza kuzaliwa kwake.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni,
Vijana na Michezo, Tabia Maulid Mwita amesema kazi kubwa inayofanywa
na Awamu ya nane ya Serikali ya Mapindizi ya Zanzibar imeiheshimisha Zanzibar
na watu wake hasa katika kuimarisha miundominu ya kisasa ya michezo.
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana amempongeza juhudi
za Serikali kwa Maendeleo makubwa yanayoendelea Zanzibar.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Fatma
Hamad Mbarouk, amesema kinachofanyika kwenye sekta ya michezo nchini ni
uimarishaji wa miundombinu imara katika kukuza tasnia ya michezo, hatua
aliyoielezea kwamba itaweka historia itakayokubukwa wakati wote na jamii.
Aidha, ameongeza kuwa Wizara ya Habari
pia itaendelea kusimamia miongozo na maelekezo wanayopokea kwa Rais Dk. Mwinyi
kwa nia ya kuleta maendeleo zaidi na kuimarisha usatawi wa jamii kupitia
michezo.
Kwa upande wake Mkandarasi Kutoka kampuni ya Orkun ilifanikisha
miradi hiyo, wameishukuru Serikali ya Mapindizi ya Zanzibar kwa kuwaamini na
kuwakabidhi kazi kubwa wanayojivunia kuikamilisha na kuikabidhisha kwa Serikali
kwa wakati.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment